Habari MsetoSiasa

Joho awashtaki wandani wa Ruto kwa kumhusisha na mihadarati

February 6th, 2019 2 min read

Na IBRAHIM ORUKO

GAVANA wa Mombasa Ali Hassan Joho ametekeleza vitisho vyake na kuwashtaki wanasiasa wanne wandani wa Naibu Rais William Ruto kwa kumhusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Bw Joho Jumanne aliwashtaki Gavana Stephen Sang wa Nandi, wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Kimani Ichung’wa (Kikuyu) na Didmus Barasa (Kimilili) kwa kumharibia jina.

Kwenye stakabadhi za kesi aliyowasilisha jana kortini, Bw Joho anadai kwamba wanne hao walinuia kumharibia jina, kumuaibisha na kumfanya achukiwe walipotoa matamshi ya kumhusisha na biashara haramu.

Anasema kwamba wanasiasa hao walitoa matamshi hayo makusudi ili kumpaka tope adharauliwe na umma.

“Washtakiwa walitoa habari za uwongo, umbea duni na lugha ya kumharibia jina na kusababisha Bw Joho achukiwe kijamii na kisiasa,” anaeleza kwenye kesi yake.

Gavana huyo anataka mahakama iagize washtakiwa kumlipa fidia kwa kumharibia jina kupitia madai ya uongo na agizo la kuwazuia wanasiasa hao, wafanyakazi na maajenti wao kuchapisha maneno ya kumharibia jina.

Bw Joho pia anataka wanasiasa hao washurutishwe kumuomba msamaha kupitia gazeti linalosomwa kote nchini. Wiki jana, gavana huyo aliwapatia wanasiasa hao makataa ya saa 24 wamuombe msamaha na kufuta kanda zote za video za matamshi hayo kwenye mitandao ya kijamii au awashtaki.

Walikataa kuomba msamaha wakisema wako tayari kukutana naye kortini.

Kabla ya matamshi hayo kutolewa, Bw Joho anasema kama kiongozi na mlezi wa vijana, alikuwa akiheshimiwa na wakazi wote wa Mombasa, wafuasi wake na magavana wenzake.

“Kufuatia matamshi hayo, heshima ya Bw Joho na maadili yameathirika pakubwa na ameibishwa sana na jina lake kupakwa tope,” nakala hizo zinaeleza.

Akiongea akiwa jijini Nairobi jana, Gavana Sang alimwambia Bw Joho kuthubutu kumshtaki akisema yuko tayari kujitetea.

Bw Sang alisisitiza kuwa ana ushahidi wa kuthibitisha kuwa Bw Joho alihusika na ulanguzi wa dawa za kulevya na yuko tayari kuuwasilisha kwa idara ya upelelezi, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na polisi wa kimataifa (Interpol) katika muda wa wiki mbili.