Habari MsetoSiasa

Joho na Balala waunga mkono marekebisho ya katiba

June 5th, 2019 2 min read

Na MOHAMED AHMED

VIONGOZI wa eneo la Pwani Jumanne waliunga mkono kura ya maamuzi ili kuwezesha kubuniwa kwa serikali inayoshirikisha Wakenya wote, na wakasisitiza kuwa eneo lao linafaa kuwa na umoja.

Wakiongozwa na Waziri wa Utalii Najib Balala na Gavana wa Mombasa Hassan Joho, viongozi hao walisema kwamba kuna haja ya katiba kufanyiwa marekebisho.

Wakiongea katika baraza la kila mwaka la Idd katika Treasury Square mjini Mombasa, ambalo lilihudhuriwa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i, viongozi wa Pwani walisema ni kupitia marekebisho ya katiba pekee ambapo usawa wa uwakilishi serikalini utaafikiwa.

“Iwapo tunataka kushirikisha kila mmoja, basi lazima tukubali katiba irekebishwe. Kama nchi, tumekuwa tukigeuza katiba tunapokumbwa na mizozo lakini kwa nini tusiibadilishe sasa tukiwa sawa,” Bw Balala alisema.

Waziri huyo alisema kwamba Rais Uhuru Kenyatta anaamini katika serikali inayowashirikisha Wakenya wote.

“Hatuna uhaba wa viongozi mashujaa. Joho anaweza kuwa kiongozi shupavu na hata mimi, lakini tunahitaji kushirikiana na jamii zote,” akasema Bw Balala.

Gavana Joho alisema kura ya maamuzi itafanyika hivi karibuni.

“Tutakuwa na kura ya maamuzi rafiki yangu, wale hawaitaki watalazimika kuungana nasi au tuwaache nyuma?” akasema.

Bw Joho alisema nchi hii ni lazima ibadilike na kuwa bora zaidi, na akawahimiza wakazi kukumbatia handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Alisema utulivu wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini unafaa kudumishwa.

“Sekta mbali mbali za uchumi wetu sasa zinanawiri kwa sababu ya utulivu. Siku zetu za usoni zinategemea uthabiti na ni sharti tupigane kuhakikisha tunaupata kwa njia yoyote inayowezekana,” alisema Gavana Joho.

Aliongeza kuwa kiongozi yeyote anayepinga umoja na vita dhidi ya ufisadi ni adui wa Wakenya.

Alishangaa ni kwa nini baadhi ya viongozi wanashtushwa na kuzinduliwa kwa noti mpya akisema ni lazima viongozi wanaopinga ufisadi waungwe mkono.

Bw Joho alizungumza baada ya viongozi kumtaka aanze mikakati ya kuunganisha eneo la Pwani wakisema anafaa kuwa kiongozi wa eneo hilo.

Vuguvuvu la Embrace Movement lilipiga jeki azma yake ya kugombea urais na kumtaka kuunganisha eneo hilo.

Viongozi wengine pwani waliohudhuria hafla hiyo wakiwemo Seneta wa Mombasa Mohammed Faki, Wabunge Ali Mbogo (Kisauni), Omar Mwinyi (Changamwe), Andrew Mwadime (Mwatate), Ken Chonga (Kilifi Kusini), Abdulswamad Nassir (Mvita) walimtaka Bw Joho kuunganisha Pwani kabla ya 2022.

“Tunakuomba uunganishe magavana wote, maseneta, wabunge na madiwani ili tuweze kuzungumza kwa sauti moja,” alisema Bw Faki.

Bw Mbogo alimhimiza Bw Joho kuongoza magavana wenzake wa eneo hilo kuunganisha wakazi.

Bw Mwadime alisema bila umoja, eneo hilo halitapata chochote.