HabariSiasa

Joho na Junet waendea 'Baba' Dubai

July 10th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

WAFUASI wa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, sasa wana matumaini kwamba hatimaye kiongozi huyo atarejea nchini hivi karibuni.

Hii ni baada ya Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, kufunga safari jana kuelekea Dubai ambako Bw Odinga alifanyiwa upasuaji majuzi.

Tangu wiki iliyopita, wafuasi wa Bw Odinga wamekuwa wakisubiri kwa hamu habari za kurudi kwake nyumbani, huku duru zikisema chama chake cha ODM kinajiandaa kumkaribisha nchini ‘kifalme’.

Matumaini yalianza kuongezeka wakati bintiye, Bi Winnie Odinga, alipotoa video iliyomwonyesha balozi huyo wa miundomsingi wa Muungano wa Afrika (AU) akiwa mchangamfu.

Mkewe, Bi Ida Odinga pia alithibitisha wiki iliyopita kwamba, mumewe anaendelea vyema na anatarajiwa kurudi nyumbani wakati wowote sasa.

Bw Joho na Bw Mohamed jana walitangaza safari yao kupitia mitandao ya kijamii.

Walipigwa picha wakiondoka katika uwanja wa ndege, na baadaye wakiwa ndani ya ndege ya kifahari ambayo haijabainika iligharimiwa na nani.

Kwa mujibu wa kampuni za kukodisha ndege, aina hiyo ya ndege ya Airbus 318 hugharibu takriban Sh500,000 kukodisha kwa saa moja pekee.

Pia, haikujulikana jinsi wawili hao waliidhinishwa kuondoka nchini ilhali kungali kuna marufuku ya safari za ndege isipokuwa za mizigo na masuala ya dharura.

“Tunaelekea Dubai na Junet Mohamed kumwona Baba,” akasema Bw Joho bila kutoa maelezo zaidi.

Tovuti ya kufuatilia safari za ndege ya FlightRadar24 ilionyesha ndege hiyo ilitoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi saa sita na dakika 45 mchana.

Ufahari wake unadhihirika kwa maelezo kuihusu, kwani ina vyumba mbalimbali vya kifahari kama vile chumba cha kubarizi, chumba cha kutumiwa na watu mashuhuri (VIP), chumba cha kulala na afisi ya kibinafsi.

Sehemu zote zimeundwa kwa vifaa vya gharama ya juu.

Bw Odinga alienda Dubai mwishoni mwa mwezi uliopita kufanyiwa upasuaji mguuni, kwa mujibu wa familia yake.

Kutokana na safari hiyo, jopo lililobuniwa kukusanya maoni kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) halijafanikiwa kuwasilisha ripoti yake iliyokamilika mwishoni mwa Juni kwa kuwa wanafaa kuiwasilisha kwa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

Safari hiyo ya Bw Odinga pia imeibua mdahalo miongoni mwa wataalamu wa siasa za kimataifa, ikidaiwa huenda anafuatilia masuala kuhusu uhuru wa Somaliland.

Taifa hilo lililojitenga kutoka kwa Somalia limekamia kutambuliwa rasmi kuwa nchi huru kimataifa, hasa kwa Milki ya Kiarabu (UAE). Bw Odinga kwa miaka mingi amekuwa akitetea wazo hilo la kujipatia uhuru.

Mjadala kuhusu nia yake halisi ya kuendelea kukaa Dubai licha ya kutangaza amepona, ulizidi baada ya Bw Mohamed, ambaye ni mwandani wake wa kisiasa, kuzuru Somaliland siku chache zilizopita.

Duru zilisema kuwa, Bw Odinga anatarajiwa kutembelea nchi hiyo hivi karibuni. Haijabainika kama amepanga kuelekea huko moja kwa moja akitoka Dubai, au atakuja Kenya kwanza.

Hayo yalitokea huku pia ripoti zikisema Chama cha ODM kimepanga kuwasilisha hoja bungeni ili Kenya itambue Somaliland kama nchi huru.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya kidiplomasia wanasema hatua hiyo itakuwa hatari kwani inaweza kuchochea zaidi uhasama kati ya Kenya na Somalia. Vile vile, itakuwa kinyume na matakwa ya sheria za kimataifa kwa Kenya kutambua nchi iliyojitenga kutoka kwa nyingine kama taifa huru.

“Kenya haiwezi kukosa busara hadi itambue nchi ambayo ilizaliwa kwa kujitenga na nyingine,” wakili Ahmednassir Abdulahi ambaye ni mmoja wa wanaofuatilia kwa karibu siasa za Somalia, akasema.