Joho ndiye chanzo cha shida zetu – Omar

Joho ndiye chanzo cha shida zetu – Omar

NA WINNIE ATIENO

WANASIASA wa mrengo wa Kenya Kwanza katika Kaunti ya Mombasa wamemlaumu Gavana Hassan Joho kwa kushindwa kulinda haki za wakazi wa Pwani.

Wakiongozwa na mwaniaji wa ugavana wa UDA, Bw Hassan Omar, wanasiasa hao walimlaumu Gavana Joho kwa uongozi mbaya, unyanyasaji na udororeshaji wa uchumi wa Mombasa.

Walidai kuwa Gavana Joho aliwaacha wafanyabiashara na wakazi wakiteseka huku uchumi wa Mombasa ukidorora.

“Bw Joho alijifanya mkombozi kumbe yeye na washirika wake wanaendelea kujali biashara zao na maslahi ya kibinafsi. Mtalipa fidia kwa yote mliofanyia wafanyabiashara na wakazi wa Mombasa,” alisema Bw Omar.

Akiongea katika mkutano wa jamii ya Wataita, Mombasa, Bw Omar ambaye alikuwa seneta, alisema gavana huyo amewasaliti Wapwani kwa kutotetea maslahi yao.

Bw Omar alisema katika miaka 10 ya uongozi wa gavana huyo, uchumi wa Kaunti ya Mombasa umefifia huku wakazi wengi wakiendelea kuwa wachochole.

Aliwaonya Wapwani dhidi ya kumuunga mkono mwaniaji wa urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga na kuwasihi kumchagua Naibu wa Rais William Ruto.

“Nitawahamasisha na kuwaelimisha Wapwani kuhusu siasa za Kenya. Kwa miaka 60 mababu zetu walikuwa wakipeleka taarifa ya makubaliano kwa serikali wakililia haki zetu, mashamba yetu, vitambulisho, mauaji ya kiholela na unyanyasaji, lakini hakuna suluhu iliyopatikana,” alisema Bw Omar.

Bw Omar alisema kinyume na Gavana Joho, atahakikisha kuwa wahudumu wa afya wanalipwa kwa wakati ufaao, ataimarisha biashara kupitia mikopo na kununua vifaa katika hospitali za umma mbali na kuimarisha sekta ya afya.

Aliyekuwa Gavana wa Taita Taveta, Bw John Mruttu ambaye anawania kiti hicho kupitia chama cha UDA aliwasihi wakazi wa Pwani kumuunga mkono Dkt Ruto ili wapate maendeleo na uchumi wa eneo hilo ufufuliwe.

Vilevile aliwasihi wakazi wa Mombasa kumuunga mkono Bw Omar.

“Bw Omar ni mtu mzuri aliye na nia nzuri kwa Wakenya, tafadhalini tumshike mkono. Napenda sera ya UDA sababu itatenga fedha za kusaidia wakulima, wafanyabaishara wadogo wadogo na wafugaji, ndio maana ni lazima tumuunge mkono Dkt Ruto,” alisema Bw Mruttu.

Alisema ana matumaini ya kushinda ugavana kwenye uchaguzi wa Agosti 9 baada ya kupenya kwenye mitaa ya Taita Taveta na kuuza sera zake.

Bw Mruttu alisema katika mipango yake atahakikisha dawa zinapatikana tena katika zahanati na hospitali za umma. “

Maanake kwa sasa wakazi wanapitia changamoto, wagonjwa wetu wanalazimika kusafirishwa kwenye magari ya wagonjwa mahututi hadi Mombasa kupata matibabu, nikichaguliwa nitaimarisha sekta ya afya,” aliapa Bw Mruttu.

Vilevile aliahidi kutoa matibabu ya bure kwa wazee wa kuanzia umri wa miaka 55 na kina mama wajawazito. Alisihi familia za Wadawida kuzaana zaidi ili kuongeza idadi yao.

  • Tags

You can share this post!

Khalwale, Echesa waahidi kupiga jeki azma ya Malala

CAF yasukuma mbele fainali za AFCON 2023 kwa mwaka mmoja...

T L