Joho, Raila wakutana kabla Azimio la Umoja

Joho, Raila wakutana kabla Azimio la Umoja

Na ANTHONY KITIMO

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, amehudhuria mkutano wa dharura na Kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, kabla ya kongamano kubwa la kinara huyo kesho.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Kaunti ya Mombasa, Bw Mudathiri Kareem, jana alithibitisha kuwa Bw Joho alielekea Nairobi kwa mkutano huo kwa jina Azimio la Umoja.Kongamano la kesho litafanyika katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Nairobi.

Bw Odinga anatazamiwa kutangaza rasmi kuwania kiti cha urais mwaka ujao.Bw Kareem alieleza kuwa safari hiyo ndiyo ilimfanya Gavana Joho, ambaye ni naibu kiongozi wa ODM, kukosa kuhudhuria kongamano la Jumuiya ya Kaunti za Pwani mnamo Jumanne katika Kaunti ya Kwale.

“Alikuwa amepanga kuhudhuria mkutano huo wa Kwale akini akalazimika kuelekea Nairobi kwa mkutano wa dharura na Bw Odinga,” akasema.Haikubainika mara moja ikiwa mkutano huo ulihudhuriwa pia na maafisa wengine wa ODM.

Kabla kusafiri kwake, Bw Joho alikuwa ameahidi kutangaza Jumatatu mwelekeo ambao angeshauri Wapwani kufuata kuelekea kwa kongamano la kesho.Duru baadaye zilisema angefanya hivyo katika kongamano la Jumuiya ya Kaunti za Pwani mnamo Jumanne, lakini hilo pia likagonga mwamba.

Hata hivyo, jana alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria kikao ambacho mabwanyenye wa Mlima Kenya walitangaza kuwa Bw Odinga ndiye chaguo lao kwa kiti cha urais mwaka ujao.“Kama una maazimio ya kuongoza nchi hii miaka ijayo, tumpigie kura Baba ili afungue njia ndipo sote baadaye tupate nafasi ya kuongoza.

Pia mimi nina ndoto ya kuwa rais lakini msipofanya uamuzi sawa hii leo, sahau ndoto yako,’ akasema Bw Joho.Awali wikendi, alikuwa amepuuzilia mbali wanasiasa ambao humtia presha ajiunge na Naibu Rais William Ruto katika chama cha United Democratic Alliance (UDA), akisisitiza kuwa yuko ngangari katika azimio la Bw Odinga.

Miongoni mwa wanasiasa hao ni Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, ambaye amepanga kuwania ugavana wa Kilifi kupitia UDA baada ya kukiasi chama cha chungwa ODM.Alipohudhuria mkutano wa kutoa tuzo za biashara bora Mombasa wikendi iliyopita, gavana huyo anayetumikia kipindi chake cha pili alifichua kuwa, tayari alimwarifu Bw Odinga kuhusu hitaji la kufanya makubaliano upya na Wapwani kuelekea uchaguzi ujao.

Bw Joho alikuwa mmoja wa wanachama waliotaka kushindania tikiti ya ODM lakini baadaye akasema atamwachia Bw Odinga nafasi hiyo.Gavana huyo hajahudhuria mikutano kadhaa ya hadhara ya ODM, ikiwemo iliyoongozwa na Bw Odinga katika kaunti za Pwani miezi ya hivi majuzi – inayovumishwa kwa kaulimbiu ya Azimio la Umoja.

Ijapokuwa Bw Odinga amekuwa akiendeleza kampeni katika pembe tofauti za nchi, huwa amesisitiza uamuzi wake kuhusu kama atawania urais au la utatokana na kile atakachosikia kutoka kwa umma kuhusu kama wanamtaka awanie wadhifa huo.

Bw Joho alikuwa mmoja wa wanachama waliotaka kushindania tikiti ya ODM lakini baadaye akasema atamwachia Bw Odinga nafasi hiyo.Gavana huyo hajahudhuria mikutano kadhaa ya hadhara ya ODM, ikiwemo iliyoongozwa na Bw Odinga katika kaunti za Pwani miezi ya hivi majuzi.

Wakati wa mwisho Bw Odinga alipozuru kaunti za Pwani kuvumisha kaulimbiu ya Azimio la Umoja, Bw Joho alikuwa katika ziara nje ya nchi na hakuna mkutano wa hadhara uliofanywa Mombasa na ODM.Baadhi ya wanasiasa wa Pwani wanaotarajiwa kuhudhuria kongamano la kesho la ODM ni wabunge, madiwani na wanasiasa wengine wanaotaka tikiti ya chama kuwania viti mbalimbali 2022.

You can share this post!

Uhuru ataacha deni la ahadi alizotoa kwenye kampeni- Ruto

Njaa: Mbunge aomba wahisani wawasaidie wakazi na chakula

T L