Habari MsetoSiasa

Joho, Waiguru, Haji, Kinoti na 'Githeri Man' watuzwa na Rais

December 13th, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kirinyaga Anne Waiguru, ni miongoni mwa magavana kumi waliopewa tuzo la heshima kuu ya taifa kwenye sherehe za Jamhuri Dei Jumatano.

Rais Uhuru Kenyatta aliwapa magavana hao pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha ODM, Bw John Mbadi, tuzo la Elder of the Golden Heart (EGH) Daraja la Pili.

Kwenye gazeti la serikali lililochapishwa Desemba 11, Rais Kenyata alisema tuzo hizo ni za “kutambua huduma bora na za kipekee zilizotolewa nao kwa taifa katika majukumu na mamlaka yao tofauti.”

Magavana wengine kwenye orodha hiyo ni Martin Wambora (Embu), Samuel Tunai (Narok), Cornel Rasanga (Siaya), Josphat Nanok (Turkana), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet), Jackson Mandago (Uasin Gishu), Dkt Alfred Mutua (Machakos) na Dkt Joyce Laboso (Bomet).

Vile vile, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai George Kinoti walitunukiwa tuzo la Chief of the Order of the Burning Spear (CBS) Daraja la Kwanza.

Wawili hao wamekuwa kwenye mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi ambavyo Rais Kenyatta amevipa kipaumbele kwenye hatamu yake ya pili ya uongozi kabla aondoke mamlakani mwaka wa 2022 inavyohitajika kikatiba.

Rais pia aliwatuza wabunge, maseneta, wanajeshi, maafisa wa polisi, wasomi, maafisa wa utawala serikalini, watumishi wa umma na raia wa kawaida waliobobea katika nyanja tofauti.

Baadhi ya wabunge waliotuzwa ni Kimani Ichungwah (Kikuyu), Shakeel Shabbir (Kisumu Mashariki), Chris Wamalwa (Kiminini), Maoka Maore (Igembe Kaskazini), na Jimmy Angwenyi (Kitutu Chache Kaskazini) ambaye ndiye mbunge mamlakani aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi, tangu mwaka wa 1994.

Kwa upande mwingine, maseneta ni Gideon Moi (Baringo), Soipan Tuya (Narok) na Johnston Sakaja (Nairobi).

Mwaka huu orodha hiyo imeonekana kuwa na tofauti kubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo wananchi wengi walilalamikia jinsi idadi kubwa ya waliopokezwa tuzo hizo zenye taadhima kubwa hawakustahili.

Malalamishi yalitokea hasa ilipobainika Bw Martin Kimotho almaarufu kama ‘Githeri Man’ alikuwa kwenye orodha, sawa na wanablogu waliochangia katika kuvumisha kampeni za Muungano wa Jubilee kabla Uchaguzi Mkuu wa 2017.

Kisheria, tuzo hizo hustahili kukabidhiwa kwa watu ambao wameonyesha ujasiri kwa manufaa ya nchi, wametoa mchango mkubwa katika nyanja tofauti zinazosaidia taifa au walioletea taifa sifa na majivuno.