Habari MsetoSiasa

Joho yu wapi? Kwa mwezi mzima 'Sultan' hasikiki

April 4th, 2018 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MASWALI yanaendelea kuulizwa kuhusu aliko Gavana wa Mombasa, Hassan Joho baada ya kukosekana kuonekana katika kaunti yake kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa wala kusikika.

Picha zilizosambaa mitandaoni zilionyesha Bw Joho akiwa katika mataifa ya bara Ulaya na Asia, lakini maafisa katika afisi yake hawakutoa maelezo ya iwapo baadhi ya ziara hizo ni rasmi au za kibinafsi.

Kama Naibu Kinara wa ODM, Bw Joho amepata umaarufu sio tu Pwani mbali maeneo mengine yenye ufuasi mkubwa wa chama hicho hasa Nyanza.

Kimya kuhusu alipo pamoja na mkubwa wake Raila Odinga kulegeza siasa kumewaacha wafuasi wao sugu na maswali tele kuhusu mwelekeo wa chama hicho.

Bw Joho alikosekana katika sakata iliyomhusu wakili Miguna Miguna huku Bw Odinga akisalia kimya kuhusu masaibu ya wakili huyo aliyerudi nchini Canada Jumapili.

Bw Miguna alipokuwa amezuiliwa katika uwanja wa ndege mjini Dubai akiwa ameugua, Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Kaunti ya Mombasa Richard Chacha alisema Bw Joho alikuwa safarini kumtembelea wakili huyo katika hospitali aliyokuwa anatibiwa lakini baadaye wakili huyo alikanusha habari hizo.

Kulingana na Bw Miguna, hawakuwasiliana na gavana huyo kuhusu mpango wa kumtembelea hospitalini.

 

Estonia

Katika ujumbe wake kwa Facebook mnamo Machi 1, Bw Joho alichapisha picha kadhaa akiwa nchini Estonia ambapo alikuwa ameandamana na baadhi ya mawaziri wake ambao walirejea nyumbani baadaye na kumuacha ugenini.

Jumanne, Taifa Leo ilimpigia simu Bw Chacha kujaribu kupata taarifa zaidi kuhusu aliko gavana huyo, lakini hangeweza kuzungumza na aliahidi kuwasiliana nasi baadaye.

Naibu Gavana wa Mombasa Dkt William Kingi amekuwa akisimamia shughuli rasmi za kaunti zikiwemo kuwapokea wageni kutoka mataifa ya nje.

Hata hivyo, kumekuwa na mgongano wa majukumu huku kisa cha hivi punde kikiwa kuhamishwa kwa baadhi ya wasimamizi wa wadi.

Diwani wa Kipevu, Faith Pendo alisema kuwa kuna baadhi ya kazi ambazo zimekwama kufuatia kutokuwepo kwa Gavana Joho.

“Bila shaka shughuli zinaendelea kama kawaida lakini kuna baadhi ya majukumu ambayo ni yeye pekee anayeweza kuyatekeleza,” alisema Bi Pendo.
Bw Kingi alisema gavana huyo yuko katika ziara ambazo zinalenga kunufaisha wakazi wa Mombasa.

 

Kazi inaendelea

“Tembelea hata Hospitali Kuu ya Pwani (CPGH) na utaona kazi inaendelea. Tumepata ufadhili mwingi kutoka Dubai,” alisema Bw Kingi na kuonya dhidi ya kuingiza siasa ziara ya gavana huyo.

Baada ya kuchapisha ujumbe wake wa Pasaka katika mitandao ya kijamii, Gavana Joho alikabiliwa vikali na wafuasi wa upinzani kwa ‘kumtelekeza’ Dkt Miguna wakati alipokuwa anahitaji ODM zaidi.

Bw Joho aliondoka nchini siku chache kabla ya Bw Odinga kukutana na Rais Uhuru Kenyatta kuafikiana wafanye kazi pamoja.

Inadaiwa Joho na mwenzake wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko walihusika sana kuwaleta pamoja viongozi hao wawili.

Siku chache baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kukutana, Naibu Rais William Ruto alizuru kaunti kadhaa za Pwani ambapo alidaiwa kulenga ushirikiano wa kisiasa na Bw Joho.

Gavana huyo baadaye alituma taarifa kwa vyombo vya habari akikanusha habari kuwa anaunga Bw Ruto kuwania urais 2022.