Habari Mseto

Joka lawasilishwa kama ushahidi

February 13th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

KULIKUWA na mshikemshike Jumatano katika mahakama ya Mombasa, maafisa wa Shirika la Kuhifadhi Wanyamapori (KWS) walipotoa joka kama ushahidi, katika kesi ya mwanamume aliyeshtakiwa kusafirisha mnyama huyo bila kibali.

Karisa Iha, 33, alidaiwa kupatikana siku ya Jumanne akiwa na joka hilo lililo na uzani wa kilo 10, katika kivuko cha feri akijaribu kulivukisha. Joka hilo lilikuwa na urefu wa mita 2.3.

Mahakama ilielezwa kuwa Bw Iha alikuwa amelihifadhi joka aina ya chatu kwenye gunia, kisha kulitia katika sanduku.

Mshtakiwa alikubali mashtaka hayo mbele ya hakimu mkazi Bw Vincent Adet.

Mafisa wa usalama waliligundua joka hilo walipokuwa wanakagua mizigo ya abiria kabla ya kuabiri feri.