Dondoo

Jombi aacha mke na kurudi kwao

March 1st, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

OLENGURUONE, NAKURU

KIPUSA aliyeolewa mwishoni mwa mwaka jana aliduwaa mumewe aliporudi kuishi na wazazi wake akidai kulemewa na maisha.

Duru zaarifu kuwa jombi alipopata jiko aliendelea kuishi na wazazi jambo ambalo lilimkosesha raha mkewe.

“Wazazi wa polo wana jumba la kifahari na jamaa aliamua kuendelea kuishi katika chumba alimokuwa akilala nyakati zake za ukapera. Polo alimtaka mkewe kusaidiana na mavyaa jikoni,” mdaku alieleza.

Mwanzoni mwa mwaka huu kipusa alimshawishi mumewe wahamie shamba ambalo walipewa na wazazi kuanza maisha yao mapya.

Baada ya muda mfupi, polo alianza kulalamika akidai majukumu ya familia yalikuwa yakimlemea akiwa na umri mdogo.

“Wazazi wangu ni masonko. Sitaki nisumbuke hadi niparare na nipinde mgongo nikiwa na umri mdogo kama huu. Afadhali turudi kwetu tulishwe na wazazi hadi tupate uwezo na namna ya kujitegemea,” polo alilia.

Inasemekana mkewe alipinga haya vikali na kumshauri mumewe kwamba bidii maishani haiumizi mtu.

“Haifai tuende tudandie mali ya wazazi. Tutumie shida hizi kama njia ya kujifunza kusaka hela. Tena, sitaki kuzomewa kila siku na mavyaa kama msichana mdogo,” kipusa alilia na kutishia kurudi kwao mumewe akishikilia msimamo huo.

Juzi, kipusa alikuwa ameenda shughuli za kusaka riziki na aliporudi alishangaa kupata lori kubwa likinguruma kwao huku vibarua wakiwa tayari wamepakia vitu hadi likajaa pomoni.

“Sirudi nyuma katika mpango wangu. Unifuate turudi nyumbani au ushike njia ya kuenda kwenu,” jombi alimwambia mkewe.