Dondoo

Jombi achekwa na marafiki kwa kukiri babake alimsaidia kuingiza demu wake boksi

April 3rd, 2024 1 min read

WERUGHA, TAITA TAVETA

Na JANET KAVUNGA

JOMBI wa hapa aliwaacha wenzake vinywa wazi alipowaeleza jinsi babake alivyomsaidia kumwingiza boksi demu aliyekuwa aking’ang’ania pamoja na rafiki yake.

Jamaa alikutana na wenzake njiani na kuwaelezea jinsi alivyokuwa na furaha tele baada ya babake kumsaidia kupata demu huyo.

“Nilidhani ndoto ya kumpata demu niliyemtamani ilikuwa imegonga mwamba kwa kuwa alinyemelewa na rafiki yangu, kumbe babangu alicheza kama yeye na sasa demu amekubali tuoane,” polo alijishasha.

Wenzake waliangua vicheko na kumkejeli wakimwambia babake ni mkali kurusha mistari kumliko.

“Yaani babako anakushinda kwa kurusha mistari hadi anamwingiza demu boksi kwa niaba yako. Unafaa kujionea huruma sana,” rafiki wa polo alisema.

***

Pasta adinda kusalimu mapolo waliomnyima kitu

MALINDI MJINI

Na JANET KAVUNGA

MAKALAMENI wa hapa walimkemea pasta mmoja kwa kukataa kuwasalimia kwa kile ambacho walishuku ni kukataa kwao kutoa sadaka alipowahubiria mtaani.

Inasemekana pasta aliwakuta makalameni katika kikao, wakamsalimia lakini akakataa kuwaamkua na kuwatupia jicho tu.
Jamaa mmoja alikasirishwa na tabia yake na akamsuta peupe.

“Pasta, kwani sisi si watu wa maana? Kwani hata salamu tu ina gharama kwako ama ni kwa vile hatukukupa sadaka juzi. Kuwa muugwana bwana, tuombee tuomoke tuweze kutoa tena kwa moyo mkunjufu,” kalameni mmoja alisema huku wenzake wakiangua vicheko.