Dondoo

Jombi achoma nguo za mke aliyemnyima asali

February 26th, 2018 1 min read

Na CORNELIUS MUTISYA

KUSYOMUOMO, MACHAKOS

KIOJA kilitokea hapa, polo alipotia kiberiti nguo za mkewe akidai alikuwa amemnyima uroda kwa muda mrefu.

Kulingana na mdokezi, polo alifunga pingu za maisha na mkewe miaka minne iliyopita na wakajaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume.

Penyenye za mtaa zaarifu kuwa, wawili hao walikuwa wakipendana kama chanda na pete hadi mama watoto alipojiunga na kanisa moja la kiroho eneo hilo na mienendo na hulka yake ikabadilika kabisa.

“Mama watoto alipoamua kuokoka, alianza kumdharau mumewe kupindukia. Alikuwa akidai alijuta kuolewa na mwanamume wa sampuli yake,’” alisema mdaku wetu.

Inasemekana kwamba, mama huyo alikuwa akishinda kanisani mchana kutwa akisingizia kuomba. Nyakati zingine alikuwa akienda katika maskani ya pasta wake kumsaidia kupiga deki nyumba na hata kumfulia nguo!

Jamaa alishuku mkewe alikuwa na uhusiano na pasta na ndio sababu alikuwa akimkausha tendo la ndoa.

Kalameni alighadhabishwa mno na mienendo ya mkewe na akaamua kufyata ulimi akitaraji kuwa siku moja atabadilika.

Hata hivyo, maji yalizidi unga mkewe alipoanza kulala katika kitanda cha watoto na akamuacha aumizwe na baridi usiku kucha. Hali iliendelea kuwa hivyo kwa muda wa miezi sita na polo akakosa uvumilivu kabisa na akaamua kuchukua hatua.

“Jombi alichukua nguo zote za mkewe na akazichoma mpaka zikawa majivu. Alitoroka na kutokomea kusikojulika,’’ akasema mdaku wetu.

Duru zaarifu kuwa polo anaendelea kusakwa na maafisa wa usalama ili akabiliwe na mkono mrefu wa sheria. Mama watoto alisomba vifaa vyote vya nyumba na akarejea alikozaliwa.