Dondoo

Jombi akemea Ex wake aliyetaka ‘wajikumbushe’

Na JANET KAVUNGA August 6th, 2024 1 min read

BOMBOLULU, Mombasa

JOMBI wa hapa alimkemea mpenzi wake wa zamani kwa kumrai ampashe joto ilhali ameolewa.

Jamaa alikasirishwa na tabia ya mwanadada huyu na akatisha kumweleza mumewe kuhusu tabia yake.

“Nilikuacha kwa sababu ya tabia yako ya kugawa asali kwa wanaume na haujaacha tabia hiyo hata baada ya kuolewa. Sitaki mambo yako na itabidi nieleze mumeo ajue tabia hii yako,” jamaa alimfokea demu ambaye alikuwa amemfuata kilabuni kumtaka wale tunda.

Demu alisisitiza haikuwa makosa kukumbuka vituko vyao vya zamani lakini jamaa akadinda kabisa na kuondoka.

***

Mambo ni mawili, ama heshimu mamangu au ufunge virago urudi kwenu, kalameni awika

GANZE, Kilifi

KALAMENI wa hapa alimwambia mkewe achague kumheshimu mama yake au afunge virango arudi kwao na kumsahau kabisa.

Jamaa alikasirika alipofahamishwa na majirani kwamba mkewe alikuwa akimdharau mamake na hata kumtusi.

Kalameni anayefanya kazi mjini Malindi alifika nyumbani na kuthibitisha madai hayo kutoka kwa mamake na watu wa familia kisha akajawa na hasira na kumchemkia mkewe.

“Mambo ni mawili; kuheshimu mama yangu ninavyoheshimu mama yako au uondoke hapa na kunisahau kama mumeo.

“Kuna wanawake wengi wenye heshima wanaotafuta wanaume waolewe na sitakuvumilia uendelee kutusi mamangu,” jamaa alilipuka hadi demu akamuomba msamaha pamoja na mamake.