Jombi alaumu mama mkwe akidai amemfilisisha

Jombi alaumu mama mkwe akidai amemfilisisha

Na TOBBIE WEKESA

NYAMACHAKI, NYERI

KALAMENI mmoja kutoka hapa, alizua kioja kwa kumlaumu mamamkwe kwa kumrudisha nyuma kimaendeleo!

Inasemekana polo alidai mama mkwe alikuwa kizingiti cha maendeleo yake maishani na kwamba alikuwa amemfanya maskini mkubwa mno kijijini.

Kulingana na polo, mara kwa mara, mama mkwe alikuwa akimsumbua akitaka msaada. “Mara anataka hiki, mara kile. Miaka nenda miaka rudi niko palepale.

Nikipanga kufanya maendeleo, utamuona na huo uzee wake akifika na kuitisha msaada,” polo alidai.

Inadaiwa mama mkwe alikuwa akifika kwa polo kila Ijumaa kuitisha msaada. Penyenye zinasema polo aliamua kumkabili mama mkwe moja kwa moja.

“Wewe kila mara huja kwangu kuitisha msaada, kwani ulimzaa msichana mmoja tu,” polo alimuuliza mama mkwe.

Mama mkwe alimuangalia polo na kumuambia mali yake ni ya binti yake. Polo alimkaripia mama mkwe huku akitisha kumtimua pamoja na binti yake.

 

Msaada

“Mali gani ya binti yako iko hapa. Kila mara unakimbia kwangu ukitaka msaada mpaka umenifilisisha. Nitakutorosha hapa pamoja na msichana wako,” polo alimfokea mama mkwe.

Polo hakumpa mama mkwe nafasi ya kujieleza. “Leo nikipanga kununua hiki, sijui huwa unatokea wapi. Mbona usinipe nafasi,” polo alimkaripia mama mkwe.

Mama mkwe alimrai polo apunguze hasira huku akiapa kutoomba kitu chochote. Inadaiwa polo alimweleza mama mkwe kuwa hatampa mahari akisema msaada wote aliompa unatosha ng’ombe watano.

“Kuanzia leo, hata na mimi ninataka kusonga mbele kimaendeleo. Tabia yako ya kuja hapa kila wakati ikome kabisa,” polo alimzomea mama mkwe ambaye alilazimika kuondoka bila kusema neno lolote.

 

You can share this post!

Kioja demu kuangua kilio baada ya bosi wake kukataa kumbusu

TAHARIRI: Serikali isiyaruhusu magenge ya uhalifu

adminleo