Dondoo

Jombi alipuka kukataliwa na demu ‘kupe’

October 6th, 2019 1 min read

Na LUDOVICK MBOGHOLI

MWANDONI, MOMBASA

JOMBI mmoja mtaani hapa aliwaka kwa hasira demu alipokataa kuzungumza naye chemba baada ya kumlipia pesa za kusukwa nywele saluni.

Yasemekana jamaa alikuwa akimmezea mate mwanadada huyo ambaye alikuwa akimhepa licha ya kumchota pesa mara kadha.

Siku ya kioja, demu alimpata jamaa akienda saluni na akamtaka amlipie gharama yote. Jamaa alikubali akitarajia kuwa angefanikiwa siku hiyo.

‘’Asante kwa kunilipia, Mungu akubariki upate zaidi ya hizo,” demu alisema akimshukuru jamaa kwa hisani yake.

“Ukiondoka unione, ninataka kuzungumza na wewe” jamaa alimwarifu demu.

Hata hivyo, demu alisema hakuwa na wakati wa kuzungumza na jamaa.

“Nikimaliziwa naenda mahali na hawa wenzangu,” alidai demu huku wenzake wakimwambia sio lazima waandamane ikiwa jamaa alikuwa akimhitaji.

“Mwenzio ana jambo muhimu anataka kukupasha, usiache riziki iende kwa mwengine,” mwanadada mmoja alimwambia demu huku jamaa akishangaa kujibiwa kwa dharau.

“Wewe ni rafiki yangu ila hatujafikia kufanya mazungumzo ya faragha,” demu alimweleza jamaa. “Si ulisema tukionana tutajadili mipango tuliyokuwa nayo, au umesahau,” kalameni alimkumbusha demu agano lao.

“Urafiki wetu ni wa kawaida, hauhusiani na masuala ya faragha, hatujawa wapenzi kiasi hicho,” alisisitiza demu huku jamaa akipandwa na hasira hadi akamkemea. “Umekuwa ukinichota pesa zangu ukiniahidi mambo usiyoweza kutimiza. Basi kama ni hivi utalipa gharama yote niliyowahi kutumia kwa mahitaji yako,” alifoka jamaa huku marafiki wa demu wakishangaa.

“Kama ni wako mbona unamfanyia hivi, wenzio wanatamani wanaume hawapati, umempata unajishebedua,” rafiki mwingine wa demu alimkaripia huku jamaa akiondoka na kuapa kwamba lazima kipusa amrudishie pesa alizotumia kwa mahitaji yake.