Dondoo

Jombi ampokonya demu TV kwa kugawa asali nje

June 19th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

MWIKI, NAIROBI

Kioja kilizuka kwenye ploti moja mtaani humu baada ya polo kugundua kwamba mpenzi wake alikuwa akimhadaa alipompata akigawa asali katika nyumba yake.

Kulingana na mdokezi, polo na mrembo walikuwa wapenzi kwa miaka miwili. Inasemekana polo aliamua kumtembelea mrembo kwa nyumba yake na alipokuwa akikaribia nyumba ya mrembo, aliamua kumpigia simu ili kumjulisha kwamba angemtembelea.

Penyenye zinasema mrembo alipokea na kumueleza polo asiende kwa sababu hakuwa nyumbani. Jamaa alishangaa kwa sababu mlango wa nyumba ulikuwa umefunguliwa na akashuku alikuwa na mtu ambaye hakutana ampate.

Inasemekana polo aliamua kuenda hadi kwa nyumba ya mrembo. Polo alimkuta mrembo ndani ya nyumba akiwa na kalameni mwingine wakiwa wameketi katika hali ya kutatanisha.

“Uliniambia nini? Unawezaje kunichezea akili. Shetani wewe,” polo alianza kumfokea mrembo. Inadaiwa mrembo naye alianza kumchemkia polo huku akimuonya dhidi ya kukanyaga kwake.

“Wewe ndiye ibilisi. Hujanioa. Ningali sokoni. Unakuja kwangu kila wakati kwani hapa ni kwako,” mrembo alilipuka.

Kutokana na hasira, polo aliamua kuichukua runinga aliyokuwa amemnunulia mrembo. “Ambia huyo jamaa uliyenaye akununulie televisheni. Pia hizo nguo umevaa nitazikujia nikampelekee dadangu,” polo alimfokea mrembo.

Penyenye zinasema polo alipoona mrembo akimlemea kwa matusi, aliamua kumzaba kofi huku kalameni aliyekuwa na mrembo akitoweka kuepuka aibu.

Jamaa hakubadilisha msimamo, alichukua chochote alichokuwa amemnunulia mwanadada huyo na kuondoka akiapa kutomrudia kwa kutokuwa mwaminifu.