Dondoo

Jombi atisha kutimua mke kwa kukataa kuamini ushirikina

March 29th, 2018 1 min read

Na LEAH MAKENA

GATUNGA, THARAKA

POLO wa hapa alitisha kumfurusha mkewe akimlaumu kwa kuchochea wanawe kutokubali dawa ya mganga ya kuwakinga kutokana na hatari.

Inasemekana kuwa polo alijulikana kwa kuamini ganga ganga za waganga na alikuwa na mazoea ya kuwaita kuwashughulikia watoto wake wakifuzu masomoni ili awape dawa ya kuwazuia na maovu wakielekea mjini kutafuta ajira.

Duru zasema kuwa awali mkewe alikuwa akishirikiana na mzee japo shingo upande ila akabadilika alipojiunga na dhehebu lililomtaka kuacha ushirikina.

Hivi majuzi, jamaa alimuita mganga kuwapa chanjo wanawe waliokuwa wakielekea mijini kutafuta kazi. Penyenye zasema jamaa alimlipa mganga huyo mbuzi watatu na akachinja wa nne kabla ya kuanza kazi yake.

Hapo ndipo mzee alijipata pekee yake kwani wanawe waliokuwa wamekomaa walidinda baada ya kushauriwa na mama yao kutojihusisha na shughuli za ushirikina.

“Wanawe walikataa katakata mipango ya baba yao huku mama yao akiwaunga mkono,” alieleza mdokezi.

Jamaa hakufanikiwa kumshawishi mkewe kukubali vidosho wake wawili wahudumiwe na mganga.

“Alimwambia kwamba alikuwa ameokoka na kamwe hangerudi kwenye shughuli za ushirikina. Wakati huo wote wanawe walikuwa wamejifungia ndani ya nyumba,” alisema mdokezi.

Baada ya vuta nikuvute kati ya jamaa na familia mganga aliamua kuondoka na zawadi zake huku akiahidi kurejea baada ya familia kuelewana.

Penyenye zasema kuwa polo alianza kumkemea mkewe huku akitisha kumtema akisema alimfanya kupata hasara kubwa.

Hatima ya mzozo huo haikujulikana japo mke na wana wa polo walishikilia msimamo wao huku jamaa akiapa kumtimua mkewe iwapo hatalegeza kamba.

…WAZO BONZO…