Dondoo

Jombi aumia mazishini aking’ang’ania chakula

May 14th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

SHIANDA, KAKAMEGA 

Kalameni mmoja eneo hili alipata majeraha usoni alipogongwa kwa sahani  na jamaa mmoja  waking’ang’ania chakula kwenye mazishi.

Yasemekana jamaa anajulikana kwa tabia ya ulafi na kudoea chakula matangani.

Hivi majuzi, alihudhuria mazishi yaliyokuwa na waombolezaji wengi.

Duru zinaarifu kwamba baada ya mazishi, waombolezaji wote walikuwa wamepanga foleni wakingoja mlo.

Foleni yenyewe ilikuwa ikisonga kwa mwendo wa konokono.

Baada ya kusimama kwa muda mrefu kwenye foleni, matumaini ya polo ya kupata kipande cha nyama yalianza kudidimia.

Aliamua kutoka kwenye foleni na kuwapita watu wote hadi eneo kulikokuwa mlo.

“Nimesimama hapa mwaka mzima. Laini haisongi na chakula kinaisha. Hebu weka hiyo nyama hapa,” polo alimkaripia jamaa aliyekuwa akigawa mlo.

Watu wote kwenye foleni walianza kumzomea polo. “Kwani wewe ni nani. Rudi kule nyuma,” watu walimfokea jamaa.

Polo hakushtushwa na kelele zao.  “Hauwezi kula mbele yangu. Toa kiwiliwili chako mbele yangu haraka,” jamaa aliyesimama karibu na polo alimkemea.

Inadaiwa polo alimuangalia tu na kujitia hamnazo.  “Wewe huoni nyama inaisha.

Karibu sufuria zinarudishwa ndani. Unataka nikose kula au nia yako ni gani?” polo alimfokea jamaa.

Habari zilizotufikia zinasema jamaa alimpa polo dakika moja  aondoke mbele yake. Polo bado alimuangalia tu. Jamaa yule alichomoa sahani yake na kumtwangwa polo kichwani.

Inasemekana purukushani zao zilisababisha wapishi kuhepa wakihofia usalama wao.

“Huyu jamaa ni mshenzi mno. Anataka kusababisha tukose chakula. Mtwange nyingine,” sauti nyingine ilisikika ikisema.

Polo alipoona sahani zinazidi kumuangukia, aliamua kuchomoka mbio.

…WAZO BONZO…