Dondoo

Jombi azomewa kwa kuoa ajuza

April 7th, 2019 1 min read

NA JOHN MUSYOKI 

MATENDENI, EMBU

JAMAA mmoja kutoka hapa alijipata pabaya alipofokewa na mama yake kwa kuoa mwanadada mzee aliyemzidi umri.

Kulingana na penyenye za mtaani, jamaa huyo alikuwa akishinikizwa na mama yake aoe ili amzalie wajukuu.

Majuzi jamaa alikata kauli na kuoa lakini cha kushangaza ni kwamba demu alikuwa wa umri mkubwa kumzidi.

Mama yake hakufurahishwa na uamuzi wa mwanawe kuoa mwanamke mzee kumzidi. Inasemekana alimsuta mwanawe na kumsihi amfukuze mwanamke huyo na kuoa mwingine.

“Mwanangu, mwanamke huyu ulimtoa wapi? Sasa ni karibu mwaka mzima na bado sijaona mke wako akiwa mjamzito. Cha kushangaza ni kuwa mke huyu uliyemuoa amekushinda kwa umri. Nadhani huenda hawezi kupata mimba kwa sababu ni mzee sana. Mpe talaka na uoe mwanamke mwingine,” mama alimwambia kijana wake.

Jamaa alimzima mama yake kwa kumdharau mke wake.

“Sasa wewe mama una shida gani? Ulikuwa unanisukuma kila siku nioe. Mke wangu ni huyu hapa.

Unalalamika kwa nini? Eti yeye ni mzee kunishinda. Sawa, nilimchagua mimi mwenyewe. Najua haja yako ni kupata wajukuu. Kuwa na subira na usiharakishe mambo. Hata kama mke wangu amenizidi umri simpi talaka,” jamaa alisikika akimwambia mamake.

Hali ilizidi kuchacha, jamaa alipokataa kubadilisha msimamo wake.

“Kwa nini unakataa maneno yangu. Hauoni aibu kuoa nyanya! Una akili timamu wewe? Ninakupa siku tatu umpe mwanamke huyo talaka aende zake. Sitaki kumuona hapa,” mama alimwambia mwanawe.

Inasemekana jamaa kwa upande wake alikaa ngumu. Hata hivyo, haikujulikana kilichojiri baada ya makataa aliyopewa na mama yake kumfukuza mwanamke huyo.