Dondoo

Jombi azuiwa kuuza kitanda cha mpenzi

December 1st, 2018 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

Machakos Mjini

KIZAAZAA kilishuhudiwa mtaani hapa kalameni mmoja alipozuiwa na wapangaji kuuza kitanda cha mpenzi wake.? Inasemekana jamaa alikuwa amezozana na kumfurusha mpenzi wake na akataka kuhama ploti.

Kulingana na mdokezi, jamaa aliamua kuuza mali iliyonunuliwa na mpenzi wake lakini akazuiwa na wapangaji kwa kuchukua hatua hiyo.

“Wewe, kwa nini unataka kuuza kitanda cha mpenzi wako. Hakuna chochote ulichonunua katika nyumba hii. Ulikuwa ukilala sakafuni hadi mpenzi wako aliponunua kitanda na sasa unataka kukiuza.

Hautauza kitanda hiki ilhali haukukinunua,” mpangaji mmoja alimfokea jamaa.? Jamaa alikanusha madai kwamba kitanda hicho kilikuwa mali ya mpenzi wake lakini alizimwa na wapangaji kabisa.

“Kinachowawasha ni nini? Nikomeni kabisa na mtu akijaribu kunizuia ataona moto,” jamaa alitisha.

Licha ya jamaa kutoa vitisho vyake, wapangaji hawakubadilisha msimamo wao kisha wakamgeukia aliyetaka kununua kitanda hicho.

“Umekuja kununua mali ya nani? Jamaa huyu hana mali. Anakuuzia mali ya mpenzi wake aliyemfurusha. Mpenzi wake alituambia tuwe macho ili asiuze mali yake. Ukinunua chochote kutoka kwa jamaa huyu utajiletea balaa,” mpangaji mmoja alimwambia mteja huyo.

Inasemekana mteja alikasirika na kuondoka baada ya mipango yake kwenda mrama. ?Jamaa aliendelea kuwafokea wapangaji kwa kuharibu mipango yake.

“Nyinyi ni watu bure kabisa. Yaani kila kitu kimeharibika kwa sababu ya uchochezi wenu,” jamaa alisema kwa hamaki.? Inasemekana wapangaji walirudisha kitanda ndani ya nyumba na kutia mlango kufuli na kumuonya jamaa vikali.

“Kama wewe ni mwanaume jaribu kuuvunja mlango wa chumba hicho. Nenda ukatafute mahali pa kulala kuanzia leo. Hautalala hapa mpaka mpenzi wako atakaporejea na kuchukua mali yake,” mpangaji mmoja alimwambia jamaa.