Dondoo

Jombi mlevi akamatwa akifuata kipusa msalani

June 5th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

TOLL, RUIRU

KIZAAZAA kilizuka katika kilabu kimoja eneo hili baada ya polo kutimuliwa alipopatikana na mabaunza katika choo cha akina dada. Kulingana na mdokezi, polo aliingia kilabuni kupigia mwili pole na baada ya kukamata chupa kadhaa, ulevi ulimlemea vilivyo.

Duru zinasema tamaa ilimuingia polo hadi akawa anawataka warembo wote kilabuni.

Penyenye zinasema polo alikuwa akisonga kutoka meza moja hadi nyingine akitaka kuzungumza na kila mrembo hadi akaamua kumfuata mmoja aliyekuwa akienda msalani.

Yasemekana mrembo aliingia ndani ya choo, naye polo akaamua kujitupa ndani ya choo kilichoshikana na kile alichoingia mwanadada huyo.

“Tafadhali msupa, naomba nambari yako ya simu,” sauti hafifu ya polo ilisikika. Kwa bahati mbaya, jamaa wawili mabaunza wa kilabu walipita karibu na vyoo vile.

“Hiyo sauti nimesikia haiwezi kuwa ya demu. Lazima kuna jamaa ameingia hapa,” baunza mmoja alimueleza mwenzake.

Duru zinasema mabaunza waliamua kumngoja polo nje.

“Boss, nani kakwambia hicho choo ni cha wanaume. Ama wewe ni mwanamke,” baunza walimchemkia polo.

Polo aliwaangalia na kujitia hamnazo. “Choo ni choo tu. Kazi ni moja. Hamuwezi kunikataza kuingia popote,” polo aliwaambia mabaunza. Majamaa nao walikasirishwa na matamshi yake ya madharau.

“Huyu jamaa hafai kuwa hapa. Anafaa kutolewa hapa. Anaingiaje choo cha akina mama na maagizo ndiyo haya pamoja na picha,” baunza alishangaa. Inadaiwa wawili hao walimuinua na kumtoa nje.

“Tunakupa dakika mbili uwe umepotea hapa,” mabaunza walimkaripia polo.

Majamaa hao walimtimua polo huku wateja waliokuwa kilabuni wakishangazwa na tabia yake.

…WAZO BONZO…