Dondoo

Jombi mlevi pabaya kutukana wakweze

March 8th, 2018 1 min read

Na CORNELIUS MUTISYA

MITABONI, MACHAKOS

POLO wa hapa alijitia mashakani alipoenda nyumbani kwa wakwe zake akiwa mlevi chakari na kuwatupia cheche za matusi akidai walikuwa wakiroga familia yake!

Kulingana na mdaku wetu, familia ya polo ilianza kukumbwa na mikururo ya nuksi na visirani. Kila wakati alikuwa akivurugana na mkewe na ikawalazimu watoto wao wahamie kwa majirani ili wapate utulivu.

“Nyumbani kwa polo kulikuwa hakukaliki. Kila siku kulikuwa kukizuka vurumai na ikabidi watoto watorokee kwa majirani,’’ alisema mdokezi.

Hivi majuzi polo alifika nyumbani akiwa mlevi na akaanza kumtusi mkewe. Vurugu zilizuka na mama watoto akafunganya virago vyake na kurudi kwao.

Inasemekana kwamba polo alienda kulala na akarauka alfajiri kwenda kwa mganga mashuhuri kupiga ramli ili amtatulie masaibu ya familia yake.

Ni mganga aliyemjulisha kwamba matatizo ya familia yake yalisababishwa na wakwe zake.

Penyenye zasema kwamba polo alipopashwa habari hizo, alikasirika sana. Alienda kwa mama pima kubugia mvinyo ili ajiliwaze nafsi. Alipiga mtindi mpaka akalewa chakari na kwa sababu ya ulevi akili ikamhadaa aende kwa wakwe zake kuwakemea kwa kuroga familia yake.

“Polo alipepesuka hadi kwa wakwe zake huku akibwabwaja maneno ya kilevi,’’ alisema mdokezi.

Kilichowakera wakwe zake hata hivyo ni polo alipoanza kuwaita wachawi akidai ndio waliokuwa chimbuko na asili ya nuksi zote za familia yake. Walitwaa nyahunyo na wakamcharaza mpaka pombe ikamtoka kichwani na akakimbia kunusuru maisha yake.

Kwa sasa, polo na mkewe wametengana kabisa huku kila mmoja akifuata njia zake.

          …WAZO BONZO…