Habari Mseto

Jomo, mwanawe Uhuru aondoa kesi aliyoshtaki serikali

February 1st, 2024 1 min read

NA SAM KIPLAGAT

MWANAWE Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta, Jomo, ameondoa kesi aliyokuwa ameishtaki serikali kuhusu mipango ya kuondoa leseni za bunduki zake.

Katika muafaka ulioidhinishwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Bw Jairus Ngaah, Bw Jomo aliondoa kesi hiyo aliyowasilisha mwaka uliopita, baada ya serikali kukubali kukoma kuingilia leseni yake ya kumiliki bunduki.

Pande husika vilevile ziliafikiana kuwa Bodi ya Leseni za Bunduki haina nia ya kuondoa leseni hiyo na kwamba itafuata kanuni zilizowekwa katika Sheria za Bunduki, kutatua suala la Bw Jomo.

“Kupitia maafikiano, suala hili limeorodheshwa kama lililosuluhishwa,” alisema Jaji Ngaah.

Muafaka huo ulisomwa na Wakili Mkuu Fred Ngatia anayemwakilisha naye wakili wa serikali, Munene Wanjohi akithibitisha uamuzi huo.

Bw Jomo alielekea kortini mnamo Julai iliyopita baada ya maafisa wa polisi kuvamia makazi yake ya Windy Ridge, Karen, mnamo Ijumaa, Julai 21 mwaka uliopita, na kumshurutisha kusalimisha bunduki zake.

Kupitia Wakili Mkuu Ngatia, Bw Jomo alihoji kuwa hatua hiyo ilikiuka haki zake kikatiba. Bw Ngatia alisema kuwa uamuzi huo ulifanywa bila kufuata mchakato uliowekwa kisheria.