Michezo

Jonkopings Sodra anayochezea nyota Eric Johana yazimwa kurejea Ligi Kuu Uswidi

December 13th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MATUMAINI ya nyota Mkenya Eric Johana Omondi kurejea kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uswidi na timu yake ya Jonkopings Sodra mwaka 2021 yamezimwa baada ya kichapo cha jumla ya mabao 4-1 kutoka kwa Kalmar, Jumapili.

Jonkopings, ambayo ilikamilisha Ligi ya Daraja ya Pili katika nafasi ya tatu, ilihitaji kulemea Kalmar iliyomaliza Ligi Kuu katika mduara hatari wa kutemwa katika nafasi ya 14, lakini haikuwa na lake nyumbani na ugenini.

Ilichapwa 3-1 Desemba 9 ugenini katika mechi ya mkondo wa kwanza ya kutafuta kupandishwa daraja kabla ya kuzamishwa kabisa katika mechi ya marudiano 1-0 Desemba 13.

Omondi hakutumiwa kabisa katika mechi ya mkondo wa kwanza, lakini alipata fursa timu hizo ziliporudiana Jumapili alipoingia katika nafasi ya Edin Hamidovic dakika ya 60.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alipata nafasi nzuri dakika ya 64 na 73. Jonkopings ilipata penalti dakika ya 82, lakini kipa akapangua mkwaju huo kutoka kwa Amir Al-Ammari.

Omondi aliwahi kucheza kwenye Ligi Kuu nchini humo akiwa mali ya Brommapojkarna mwaka 2018. Brommapojkarna ilitemwa msimu huo ilipokamilisha ligi hiyo ya timu 16 katika nafasi ya 14.

Mabeki Joseph Okumu na Eric ‘Marcelo’ Ouma wanasakata soka yao ya malipo katika klabu za Elfsborg na AIK ambazo zilikamilisha Ligi Kuu 2020 katika nafasi ya pili na tisa, mtawalia.