NA CHARLES WASONGA
JOPO la kuteua mwenyekiti na makamishna limewahakikishia Wakenya kwamba litaendesha shughuli hiyo kwa njia ya haki, yenye uwazi na isiyopendelea.
Kwenye kikao na wanahabari katika jumba la KICC, Nairobi mnamo Jumatano, Machi 15, 2023, mwenyekiti wa jopo hilo Nelson Makanda alisema kuwa yeye na wenzake watazingatia Katiba na sheria husika wakitekeleza kibarua hicho muhimu.
“Kwa hivyo, tunawaomba Wakenya waliohitimu waendelea kutuma maombi yao kwa wadhifa wa mwenyekiti na makamishna sita wa IEBC tulivyotangaza wiki jana. Tunawahakikisha kuwa wale ambao tutampendekezea Rais watakuwa ni watu waliohitimu na watakaotekeleza kazi hiyo kwa uadilifu,” akawaambia wanahabari aliopokuwa akielezea hatua ambazo jopo hilo limepiga kufikia sasa katika shughuli hiyo.
Dkt Makanda alisema hayo wakati ambapo muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya ukishikilia kuwa hautatambua kazi ya jopo hilo.
Kiongozi wa muungano huo Raila Odinga anasema kuwa mrengo wake hauna imani kwa utendakazi wa jopo hilo kwa sababu “wanachama wake wote wanaegemea mrengo wa Kenya Kwanza.”
“Hii ni jopo ambalo liliteuliwa na Ruto na hivyo sisi kama Azimio hatuliamini. Tunataka shughuli ya uteuzi wa makamishna wa IEBC uendeshwe kwa njia inayoshirikisha wadau wote,” akasema Bw Odinga katika mkutano wa Azimio Jumanne mjini Siaya.
Lakini Jumatano, Bw Makanda alisema kuwa jopo lake pia litafanya mashauriano na wadau mbalimbali katika mchakato mzima wa uchaguzi ili kukusanya kauli zao.
“Mashauriano na madau ni mojapo ya mbinu ambayo tutatumia kuvutia ukabalifu kutoka kwa wadau na Wakenya kwa ujumla,” akaeleza.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa kifikia Jumatano jumla ya Wakenya 169 walikuwa wametuma maombi kwa nyadhifa za mwenyekiti na makamishna wa IEBC.
“Wakenya bado wako na muda wa hadi Machi 28, 2023 kutuma maombi yao,” Bw Makanda akasema.