Habari Mseto

Jopo lasaka soko la miraa Djibouti na Msumbiji

June 19th, 2019 2 min read

DAVID MUCHUI na GITONGA MARETE

JOPOKAZI lililobuniwa kutekeleza mapendekezo ya ripoti kuhusu jinsi ya kuboresha soko la miraa sasa linataka Kenya kuuza zao hilo nchini Djibouti na Msumbiji.

Wawakilishi wa jopokazi hilo lenye wanakamati 23, wako nchini Ethiopia ili kujifunza jinsi ya kuboresha biashara ya miraa.

Kiasi kikubwa cha miraa inayotumiwa nchini Somalia inatoka Ethiopia.

Chama cha Wakuzaji wa Miraa cha Nyambene (Nyamita) pia kimeanzisha kampeni ya kuhakikisha kuwa zao hilo linauzwa katika soko la humu nchini.

Kupitia barua yake kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni, mwenyekiti wa jopokazi hilo Kello Harsama, ujumbe wa watu wanane utazuru Ethiopia, Djibouti na Msumbiji.

Bw Harsama alisema jopokazi hilo litahakikisha kuwa Wakenya wanaokuza miraa wanapata masoko ya kutosha ya kuuza zao lao.

“Jopokazi litazuru Ethiopia, Djibouti na Msumbiji kwenda kusaka soko la miraa. Tutazuru wizara za kilimo, idara za usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi, vyama vya wafanyabiashara ili kujifahamisha kuhusu matakwa ya kuingiza katika nchi hiyo miraa,” akasema Bw Harsama kupitia barua yake kwa wizara.

Kulingana na Bw Kimathi Munjuri ambaye ni mmoja wa wanajopo walio ziarani kusaka soko, tayari wamekutana na chama cha wafanyabiashara wa miraa nchini Ethiopia ili kufahamu jinsi ya kukabiliana na ushindani katika soko la zao hilo.

“Tumekutana na chama cha wafanyabiashara wa miraa. Tunatarajia kukutana na maafisa wa serikali kuu na serikali ya mkoa ili kufahamu jukumu la serikali katika biashara ya miraa,” akasema Bw Munjuri.

Alisema wakulima nchini Ethiopia wanakuza zaidi ya aina 50 za miraa.

Miraa ya Ethiopia inauzwa kwa wingi nchini Somalia na Djibouti na huiletea kiasi kikubwa cha mapato.

Wakulima wa Kenya wamekuwa na kibarua kigumu kuingiza miraa katika soko la Somalia ambalo limefurika bidhaa hiyo kutoka Ethiopia.

Inakadiriwa kuwa Ethiopia hupeleka zaidi ya tani 16 za miraa nchini Djibouti kila siku. Ethiopia hupata ushuru wa Sh1.7 bilioni kila mwaka kutokana na miraa.

Miraa imeharamishwa nchini Msumbiji lakini jopokazi hilo linasema kuwa huenda likawa soko kubwa endapo itahalalishwa.

Mnamo 2017, Mamlaka ya Kilimo na Vyakula (AFA) ilisema kuwa ilikuwa ikiendelea na mikakati ya kusaka soko la miraa nchini Sweden, Norway na Israeli.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wakuzaji wa Miraa nchini (Kemifata) Peter Kinyua alisema kuwa kuna uwezekano wa kupata soko la miraa nchini Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Botswana na China.