Michezo

JOPO LAUNDWA: Lawajibishwa na jukumu la kuweka mustakabali mwema klabuni AFC Leopards

July 17th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

WANACHAMA na washikadau wa klabu ya AFC Leopards wameteua jopo la watu 10 kusimamia klabu hiyo kwa muda hadi uchaguzi utakapofanyika mwezi Septemba, siku chache baada ya mkutano maalum.

Walioteuliwa ni Alex Ole Magelo, Maurice Amahwa, Oscar Igaida, Richard Ekhalie, Maurice Osundwa, Boniface Ambani, Robert Asembo, Dan Shikanda, Susan Wamalwa na Timothy Lilumbi.

Hatua hii imechukuliwa baada ya Msajili wa Michezo Kenya kukataa kuidhinisha afisi mpya iliyochaguliwa majuzi kuongoza klabu hiyo ya ligi kuu ya Kenya (KPL).

Rose M N Wasike alikataa kupokea na kuidhinisha majina ya watu watatu waliochaguliwa mwezi uliopita kwa madai kwamba klabu hiyo haijatimiza mambo muhimu kuambatana na Sheria Mpya za Michezo.

Wasike alisema watu wapatao 500 walioshiriki kwenye zoezi hilo katika Uwanja wa Kimataifa wa MISC, Kasarani walipuuza agizo la katibu mpya wa michezo.

Hii ni kinyume na agizo la Wasike ambaye alikuwa ameishauri afisi ya Ingwe kuahirisha uchaguzi huo ili wapate wakati kufanya uchaguzi wa haki na kuaminika kuambatana na kanuni za uchaguzi.

Kulingana na sheri mpya, shirika lolote lazima lifanye uchaguzi kuambatana na Kifungu cha 81 cha katiba ya Kenya mpya ya 2010 kuhusianana na Sheria za Michezo na Masharti.

Orodha ya wanachama

Katika barua aliyowaandikia viongozi wa AFC Leopards SC, Wasike alitaka klabu hiyo impatie orodha ya wanachama halisi waliojiandikisha kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo (2017, 2018 na 2019) kutoka angalau Kaunti 24 ili washiriki kwenye uchaguzi huo, lakini wakakosa kutoa orodha hiyo.

Kadhalika, afisi kuu ya klabu hiyo iliagizwa kufutilia mbali majina ya watu walioteuliwa kusimamia shughuli hiyo baada ya utata kutoka kwa wanachama waliodai kwamba majina yalitolewa kwenye orodha ya wapigakura.

Kamati hiyo ya kusimamia uchaguzi iliuendesha uchaguzi huo ambapo wanachama walimchagua Dan Shikanda kama mwanachama mnamo Juni 23.

Wengine waliochaguliwa ni Oliver Sikuku kama Katibu Mkuu mpya na Maurice Choge Chichi kama mweka hazina. Hali hii ilikuwa imekiweka hatarini klabu ya AFC Leopards ambayo ilikaribia kupigwa marufuku pamoja na wote waliochaguliwa kwa kupuuza agizo la katiba ya Kenya.