Habari Mseto

Jopo linalomchunguza Jaji Ojwang kuzuru makazi yake

June 18th, 2019 1 min read

Na Richard Munguti

JOPO linalomchunguza Jaji wa Mahakama ya Juu Jackton Ojwang aliyesimamishwa kazi kwa madai ya utovu wa nidhamu litazuru barabara inayodaiwa alijengewa kwa kutupa kesi ya shamba.

Jopo hilo linaloongozwa na Jaji Alnashir Visram, wa Mahakama ya rufaa litaenda kujionea barabara hiyo, ambayo Jaji Ojwang anasema inatumikia umma kabla ya kuanza kupokea ushahidi Julai 15, 2019.

Na wakati huo huo Jaji Ojwang aliomba jopo hilo lipokee ushahidi faraghani ijapokuwa anadumisha hakuna makosa aliyofanya kustahili kutimuliwa kazini.

Iwapo jopo hilo litampata na hatia basi, litampendekezea Rais Uhuru Kenyatta amfute kazi Jaji Ojwang , ambaye ni mmoja kati ya majaji saba wa mahakama ya upeo.

Mbali na dai hilo la kufaidika kwa barabara, kuna madai mengine mawili dhidi ya Jaji Ojwang ambayo ni kwamba alikaidi kufika mbele ya tume ya kuajiri watumishi wa mahakama (JSC) na dai la tatu ni kuwa aliidharau tume hiyo.

Kuhusu barabara , Jaji Ojwanga adaiwa alijengewa barabara hiyo na Gavana wa Migori Okoth Obado.

Jopo hilo litapokea ushahidi katika kijiji cha Uriri ambapo Jaji Ojwang ametoka na amejenga nyumba.

Barabara ambayo Jaji Ojwang adaiwa alijengewa ni Kakrao – Rayudhi-Ojele.

Mbali na Jaji Visram wanachama wengine wa jopo hilo ni

Jaji (mstaafu) Festus Azangalala, Ambrose Weda, Andrew Bahati Mwamuye, wakili Lucy Kambuni, Sylvia Wanjiku Muchiri na Amina Abdalla.

Wakili Paul Nyamodi atakuwa akisaidia jopo hilo kuwasilisha ushahidi na masuala mengine.