Habari Mseto

Jopo maalum kuundwa kufanikisha muafaka wa Uhuru na Raila

April 22nd, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila amesema yeye pamoja na Rais Uhuru Kenyatta watabuniwa jopo maalum litakalowashauri kuhusu jinsi ya kuunganisha nchi kwa manufaa ya Wakenya wote.

Wanachama wa jopo hilo pia watawaelekeza wawili hao kuhusu namna na kuzuia machafuko ya kisiasa ambayo yamekuwa yakishuhudiwa nchini kila baada ya uchaguzi.

Akiongea Jumamosi eneo la Bondo alikohudhuria hafla mazishi, Bw Odinga alielezea matumaini kuwa utaratibu huo utasaidia kusuluhisha shida ambazo zimekuwa zikilizonga taifa hili tangu uhuru.

“Tunataka kujadiliana ili kupata masuluhisho ambayo yatashughulikia mahitaji yetu. Hatutaki kuandaa uchaguzi mwingine ambao utatugawanya kama Wakenya,” akasema.

Bw Odinga aliwaambia waombolezaji kuwa Kenya inahitaji kuweka ambao utaisaidia kuafikia maendeleo katika nyanja zote kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vile vya siku zijazo.

Alisema ataendelea kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali nchini katika juhudi zake za kupalilia umoja na utangamano nchini.

“Ndoto yangu kuu ni kuunganisha nchi, bila masharti yoyote. Hii ndio maana baada ya kukutana na Rais Kenyatta na kukubaliana kuzika tofauti zetu za kisiasa, nimekuwa nikikutana viongozi wakuu nchini. Nitaendelea kufanya mikutano kama hiyo,” akasema.

Mnamo Ijumaa Bw Odinga alifanya mashauriano na Rais mstaafu Mwai Kibaki nyumbani kwake (Kibaki) katika mtaa wa Muthaiga. Mkutano huu unajiri wiki moja baada ya kiongozi huyo wa upinzani alienda Kabarak, Nakuru kufanya mashauriano na Rais mstaafu Mzee Daniel Moi.

Viongozi wengine ambao Bw Odinga amewahi kukutana nao afisini mwake jumba la Capital Hill, Nairobi ni Gavana Mike Sonko na aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo.