Michezo

Jose Mourinho aweka wazi azma yake Spurs

July 27th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Jose Mourinho amesema analenga kuwarejesha Tottenham Hotspur “wanakostahili kuwa” baada ya kuwaongoza kufuzu kwa soka ya Europa League msimu ujao wa 2020-21 licha ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Crystal Palace uwanjani Selhurst mnamo Julai 22, 2020.

Matokeo hayo yaliwasaidia Tottenham kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu katika nafasi ya sita kwa alama 59, mbele ya Wolves waliozamishwa 2-0 na Chelsea ugani Stamford Bridge. Licha ya kujizolea jumla ya alama 59 sawa na Tottenham, Wolves walioorodheshwa katika nafasi ya saba kutokana na uchache wa mabao yao.

“Wachezaji wote wanapokuwa katika hali shwari ya kuchezeshwa, tumedhihirisha kwamba tuna uwezo wa kurejea tunakostahili kuwa kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza na soka ya bara Ulaya. Sioni sababu yoyote itakayotuzuia kukamilisha kampeni za msimu ujao ndani ya mduara wa tatu au nne-bora kwa sababu huko ndiko tunakostahiki kuwa,” akatanguliza kocha huyo wa zamani wa Man-United, Chelsea, Benfica, Inter Milan na Real Madrid.

“Nahitaji kuwa na kikosi thabiti cha wachezaji walio tayari kuwajibishwa wakati wowote. Sitaki kuwa na chumba cha wachezaji wagonjwa. Nataka kuwa na uwanja uliojaa wachezaji walioko katika fomu nzuri kila wanaposhuka dimbani,” akaongeza kwa kusisitiza kuwa lengo lake kuu kwa sasa ni kudumisha wanasoka wake wote tegemeo na kujishughulisha kidogo kwenye soko la uhamisho kadri anavyopania kukisuka upya kikosi chake.

“Tunaenda kununua wachezaji 10 wapya? Hapana. Tunaenda kununua wachezaji kwa kima cha Sh14 bilioni? La hasha! Tunapania tu kuimarisha na kuboresha kikosi kilichopo kwa sasa,” akaongeza.

Harry Kane aliwaweka Tottenham kifua mbele kunako dakika ya 13 baada ya kushirikiana na Giovani lo Celso kabla ya Jeffrey Schlupp kusawazishia Crystal Palace katika dakika ya 53.

Matokeo hayo yalikomesha rekodi duni ya Palace ambao chini ya kocha Roy Hodgson, walishuka dimbani wakiwa wamezidiwa maarifa katika mechi saba mfululizo ligini. Palace walifunga msimu katika nafasi ya 14 kwa alama 43.