Makala

JOSEPH MWANGI: Chipukizi aliyezindua mtindo mpya wa 'Dabonge'

March 22nd, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

NI mwimbaji na produsa anayeibukia katika ulimwengu wa muziki wa burudani. Anasema anapania kujituma kwa udi na uvumba kuhakikisha anatinga upeo wa kimataifa miaka ijayo.

Joseph Mwangi maarufu Jobi mdabonge anasema ingawa hajapiga hatua kubwa katika muziki analenga kuibuka staa.

”Nilianza utunzi wa nyimbo zangu mwaka 2009 ambapo nimebahatika kughani fataki kadhaa,” anasema na kuongeza kuwa jukwaa la muziki sio mteremko.

Chipukizi huyu ambaye pia ameanza kupiga picha za video anasema yeye ndiye mwanzilishi wa mtindo mpya unaoitwa ‘Dabonge’.

Anasema anataka mtindo huo uwe ndio unaotumika na wasanii wa hapa Kenya kama ilivyo nchini Tanzania ambapo hutumia mtindo wa Bongo na Uganda ambayo wasanii nchini humo hutumia Dance hall.

Dabonge ndiyo mtindo uliotumiwa na kundi la wasanii la Sailors lililotunga nyimbo iitwayo ‘Wamlambez’ iliyozua msisimko zaidi hapa nchini miongoni mwa vijana ambao ndio wafuasi wa nyimbo za kizazi kipya.

Kijana huyu anasema anataka kufikia kiwango cha waimbaji wa Bongo Fleva kama Roma Mkatoliki na Nay wa Mitengo kati ya wengine.

Chipukizi huyu ameghani na kurekodi nyimbo kama ‘Mijimiji’ aliyotunga mwaka 2012. Anasema teke hiyo ilimsaidia pakubwa katika ujio wake maana ilimpa nafasi kufanya shoo nyingi tu hapa nchini pia nchini Tanzania.

”Nyimbo hiyo ilinipiga jeki zaidi katika masuala ya muziki maana kati ya mapato yake yamenisaidia kufikia nilipo kwa sasa,” alisema na kuongeza kuwa aliitumia pakubwa kuwapigia debe wanasiasa mbali mbali kuelekea uchaguzi wa mwaka 2013.

Kando na nyimbo hiyo pia ametunga nyimbo zingine ikiwamo: ‘Mungu nisamehe,’ ‘Gospel Anthem,’ na ‘Mungu mbele.’ Pia ndani ya miaka miwili iliyopita ametunga nyimbo mbili ‘Kaundu heho,’ na ‘Mkali wao.’

Mwangi anamiliki lebo ya kurekodi muziki kwa jina Bashment Records aliyoanzisha mwaka uliyopita mtaani Huruma Nairobi.

”Nilianzisha lebo yangu ili niweze kujifunza namna ya kurekodi nyimbo nzuri zinazoweza kupata mpenyo kupeperushwa na vyombo vya habari nchini,” anasema.

Kufikia sasa anajivunia kurekodi kazi za zaidi ya wasanii kumi wanaokuja hapa nchini. Chipukizi huyu amerekodi nyimbo za wasanii kama Mzito far ‘Siwezi solo,’ Hyper gang ‘Vitu mature,’ Santo boy ‘Vumilia,’ Nutty-Congo ‘Kayau,’ Sunpack, Humble G na Pekari and Dan Dogo kati ya wengine.

Katika mpango mzima anasema analenga zaidi kuona muziki wa Kenya unakubalika na wapenzi wa burudani.

Pia anapania kukuza talanta za wanamuziki chipukizi nchini hasa kutoka makao ya watoto yatima.

”Kusema kweli hakuna asiyependa kuwa maarufu kwa jambo analofanya kwa hivyo ningetaka zaidi kufikia hadhi ya maprodusa mahiri nchini kama Maji Kenga kati ya wnegine,” alisema na kuongeza kwamba anafahamu hakuna jambo nzuri huja rahisi ambapo lazima ajitume kama mchwa.

Anasema kabla ya kuanzisha lebo yake alipitia pandashuka nyingi tu ikiwamo ukosefu wa fedha kurekodi nyimbo nzuri.

Pia katika ujio wake alikubana na hali ngumu hasa vyombo vya habari kutocheza nyimbo zake.