Habari Mseto

Joshua Kipkorir na Priscah Cherono ni miongoni mwa wakimbiaji 50,000 watakaoshiriki Standard Chartered Singapore Marathon

November 29th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Joshua Kipkorir na Priscah Cherono wako katika orodha ya wakimbiaji 50,000 kutoka mataifa 133 wanaotarajiwa Jumamosi kushiriki mbio za kilomita 42 za Standard Chartered Singapore Marathon nchini Singapore.

Mabingwa Kipkorir na Cherono wamerejea jijini Singapore kutetea mataji yao baada ya kuyanyakua kwa saa 2:12:18 na 2:32:11 mwaka jana, mtawalia.

Kipkorir aliendeleza utawala wa Kenya katika kitengo cha wanaume cha Singapore Marathon hadi miaka 17 mwaka 2018 naye Cherono alikuwa Mkenya wa nne mfululizo kutwaa taji la kinadada.

Katika makala ya mwaka huu, Kipkorir anatarajiwa kupata ushindani mkali kutoka kwa watimkaji kutoka Kenya, Ethiopia, Bahrain na Morocco.

Naye, Cherono atakuwa na kibarua kigumu kuhifadhi taji lake, hasa baada ya kitengo cha wanawake kuvutia bingwa wa Sydney Marathon Stella Barsosio (Kenya) pamoja na Mamitu Daska (Ethiopia) na Mbahraini Merima Mohammed, ambao wanatarajiwa kumkosesha usingizi.

Wakimbiaji tatu-bora watazawadiwa Sh5.1 milioni, Sh2.6 milioni na Sh1.5 milioni, huku nafasi ya nne hadi 10 ikiandamana na tuzo ya kati ya Sh1.0 milioni na Sh102,560