Michezo

Joshua na Pulev kuvaana katika pigano kali la masumbwi ugani Wembley

December 12th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

ANTHONY Joshua amewataka mashabiki wake kutarajia makuu atakaposhuka ulingoni kuchapana na Kubrat Pulev leo Disemba 12, 2020, katika ukumbi wa Wembley Arena, Uingereza.

Walipoonana mnamo Disemba 11, 2020 katika shughuli ya kukagua ulingo, mabondia hao walirushiana cheche za maneno huku Pulev ambaye ni bingwa wa dunia katika uzani wa heavyweight akimfokea Joshua na kumwita ‘mtoto mdogo asiye na adabu’.

Kwa upande wake, Joshua alimwonyeshea Pulev kidole na nusura amzabe kofi kabla ya walinzi kuingilia kati.

“Ningemzaba kofi kali la shavuni mara hiyo hiyo. Lakini walinzi waliniambia nisubiri hadi Disemba 12 ambapo ndiyo siku ya pigano,” akasema Joshua, 31.

Akihojiwa na wanahabari, Joshua ambaye ni raia wa Uingereza alisema asingerudia runingani maneno ambayo alimtupia Pulev.

“Kwa miaka mingi ambapo nimekuwa katika ulingo wa ndondi, nimeona wanamasumbwi wengi wakizungumza kwa makeke na kurusha matusi. Aibu ni kwamba wanaozungumza sana kwa kujidai huishia kuchapwa vibaya sana,” akasema Joshua.

“Najua Pulev alivyo. Nimemsoma. Anadhani kwamba yeye ni tisho na shujaa. Nimemwambia mara kadhaa asitumie rekodi za ufanisi wa awali kujitapa kwa sababu mimi si sawa na hao aliowadhalilisha,” akaongeza Joshua.

“Wapiganaji wanaposhuka name ulingoni, huwa wakijivuna na kujiamini sana. Lakini baada ya raundi chache za mchapano, hujipata hoi kabisa,” akaongeza.

Pulev ambaye ni raia wa Bulgaria atashuka ulingoni akiwa na uzani wa 239.7lbs (kilo 108.7) baada ya kupunguza uzani wa 9lbs (kilo 4.08) tangu ashiriki pigano la mwisho. Kwa upande wake, Joshua kwa sasa ameongeza uzani wa 4lbs (kilo 1.81) kutoka kwa uzani wa 240.8lbs (kilo 109.2) aliokuwa nao mara ya mwisho alipochapana na Andy Ruiz mnamo Disemba 2019.

Joshua na Pulev walikuwa wameratibiwa kuchapana makonde katika uwanja wa Tottenham Hotspur jijini London, Uingereza mnamo Juni 20, 2020 kabla ya mchapano huo kuahirishwa kwa sababu ya corona.

Kwa mujibu wa Matchroom Boxing ambao ni mapromota wa Joshua, yalikuwa matamanio yao kufanikisha pigano hilo uwanjani ugani Tottenham.

Joshua hajashiriki ndondi zozote tangu Disemba 2019 baada ya kumzidi maarifa Andy Ruiz Jr kwa wingi wa alama nchini Saudi Arabia. Mchapano huo ulimpa Joshua jukwaa maridhawa la kurejesha ufalme aliokuwa amepokonywa hapo awali na mwanamasumbwi huyo mzawa wa Amerika na raia wa Mexico jijini New York, Amerika mnamo Juni 2019.

Pulev atakuwa akiwania fursa ya kutwaa taji la IBF kutoka kwa Joshua ambaye pia ni mshikilizi wa mataji ya dunia ya WBA na WBO. Awali, wawili hao walikuwa wamepangwa kumenyana mnamo Oktoba 2019 uwanjani Cardiff Principality, Uingereza. Hata hivyo, Pulev alijiondoa katika dakika za mwisho baada ya kupata jeraha baya la bega.

Eddie Hearn ambaye ni promota wa Pulev amesema bondia wake yuko ange kwa pigano hilo litakalohudhuriwa na zaidi ya mashabiki 1,000.

Ushindi kwa Joshua utampa fursa ya kuvaana na Mwingereza mwenzake Tyson Fury ambaye ni mshikilizi wa taji la WBC la uzani wa ‘heavy’.