Makala

Joto kali Sudan Kusini lasukuma serikali kufunga shule

March 18th, 2024 1 min read

LABAAN SHABAAN na MASHIRIKA 

SUDAN Kusini imefunga shule zote kuanzia Jumatatu, Machi 18, 2024 ili kulinda wanafunzi dhidi ya wimbi la joto kali.

Joto hilo linalotarajiwa kudumu kwa wiki mbili linatarajiwa kuongezeka hadi nyuzi joto 45.

Wizara ya Afya na ile ya Elimu nchini humo imeshauri wazazi kuwaweka watoto wote ndani ya nyumba katika kipindi hiki.

Onyo kali limetolewa kwa shule yoyote itakayokiuka maelekezo.

Hatua za kisheria, ikiwemo kupokonywa leseni ya kuhudumu, itawakabili wasimamizi wa shule watakaokaidi amri ya serikali.

Taarifa iliyotolewa mnamo Jumamosi, Machi 16, 2024 haikubainisha shule zitafungwa kwa muda upi.

“Tutaendelea kufuatilia hali hii na kujulisha umma ipasavyo,” ilisema taarifa ya serikali.

Mkazi Peter Garang, anayeishi katika mji mkuu, Juba, alifurahia uamuzi huo.

Alisema: “Shule ziunganishwe kwenye gridi ya umeme ili kuwezesha ukitaji wa viyoyozi vya kupoza hewa.”

Sudan Kusini, mojawapo ya mataifa machanga zaidi duniani, huathirika zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mawimbi ya joto huwa ya kawaida lakini mara chache huzidi nyuzi joto 40.

Ni nchi ambayo inaendelea kukumbwa na majanga mengine kama vile athari za mizozo ya wenyewe kwa wenyewe.

Kadhalika, vipindi vya ukame na mafuriko hufanya hali ya maisha kuwa magumu kwa wananchi.

Waziri wa Afya, Yolanda Awel Deng ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Elimu amewataka wananchi kutahadhari kwa sababu mawimbi ya joto kupita kiasi husababisha hatari kubwa kiafya.

Hali hii huleta mkazo mwingi wa kisaikolojia kwenye mwili wa binadamu.

Pia inaweza kuchochea vifo kwa kuzidisha shinikizo ya magonjwa ya kupumua, ya moyo na ya mishipa.