Siasa

Joto kuhusu mgombea wa urais wa Azimio lashamiri mazishini

February 10th, 2024 2 min read

KITAVI MUTUA Na CHARLES WASONGA

MJADALA kuhusu nani anafaa kupeperusha bendera ya Azimio La Umoja-One Kenya katika uchaguzi mkuu ujao wa urais ulishamiri Jumamosi katika mazishi ya shemejiye kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Kaunti ya Kitui.

Kinara muungano huo Raila Odinga aliamua kueleza mikakati ya kisiasa ya kukubaliana kuhusu mgombeaji mmoja wa urais atakayepambana na Rais William Ruto mwaka 2027.

Alikabiliana na suala hilo ambalo limegeuka kiazi moto katika Azimio kwa kuhakikishia jamii ya Wakamba kwamba haoni ugumu wowote kujiondoa na kuidhinisha Bw Musyoka kwa wadhifa huo mkuu nchini.

Aidha, alieleza kuwa ndani ya Azimio kila moja ya vyama tanzu 26 kina usemi wake ambao lazima ushirikishwe kwenye maamuzi muhimu kama hayo.

Bw Odinga alikariri kuwa Bw Musyoka amechangia pakubwa katika majaribio yake (Raila) ya kuingia Ikulu, mara tatu, na anayo haki ya kutunikiwa tiketi hiyo.

Hata hivyo, aliwataka watu wa eneo hilo na Wakenya kwa ujumla kuwa watulivu “kwani uamuzi huo utafanya kwa makini zaidi.”

“Siwezi kuwa kiongozi asiyeshukuru kwa wema aliyotendewa kwa kutambua kuwa Kalonzo aliniunga mkono mara tatu; 2023, 2017 na 2022,” Bw Odinga akasisitiza.

Lakini wandani wa Bw Musyoka hawakushawishika na hakikisho hilo, wakisema jamii imepoteza katika mikakati ya kisiasa ya kuteua mpeperushaji bendera ya urais kupitia mrengo huo.

“Wengi hawafahamu kuwa familia yangu ina ushirika mkubwa na familia ya Bw Kalonzo. Tumetoka mbali naye na urafiki wetu unavuka mashindano ya vyama vyetu vya kisiasa,” Bw Odinga akaeleza.

Kiongozi huyo wa upinzani hata hivyo alionya kuhusu madhara ya kutaja mgombeaji wa urais wa Azimio mapema akisema hatua hiyo huenda ikaugharimu muungano huo kisiasa.

Mazishi ya mwendazake, Mzee Willy Muasya, yalifanyika eneo la Kasaala Ikutha.

Alivishauri vyama tanzu katika Azimio kuendeleza mchakato wa kujiimarisha ili viwe na nguvu, baada ya kuitisha presha ya kutangaza mgombeaji wao wa urais mapema.

“Wakenya wasiwe na wasiwasi wanapoona Wiper, ODM, PNU au chama chochote cha upinzani kikishiriki katika shughuli tofauti za kisiasa. Wiper yenye nguvu huchangia muungano wenye nguvu wa Azimio,” akaleza.

Lakini viongozi waliochaguliwa kutoka eneo hilo wakiongozwa na magavana walipuuzilia mbali kauli za Odinga wakibashiri Azimio itashindwa tena 2027 ikijivuta kutangaza mgombeaji wake wa urais.

Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Junior alisema Azimio inafaa kujichukulia kama serikali mbadala na kutangaza mgombeaji wao wa urais mapema kumpa muda tosha wa kuendesha kampeni kote nchini.

Bw Kilonzo alisema hiyo ndio ya kipekee ya kuibua matumaini na kuwaleta pamoja wakifahamu kuwa wanayo serikali mbadala na mgombeaji urais ambaye yu tayari kuangusha Rais Ruto na Kenya Kwanza.

“Hii ni muhimu kwetu katika Wiper kwa sababu hatuwezi kuiruhusu Azimio kusubiri hadi Julai 2026 kuanzisha shughuli ya aibu ya kuwaita wagombeaji kwa mahojiano kubaini anayefaa huku tarehe ya uchaguzi ikikaribia,” Gavana huyo wa Makueni akaeleza.

Naye seneta wa Kitui Enock Wambua alisema suala la mgombeaji wa urais wa Azimio sharti liamuliwe kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2024.

Mjadala huo ulianzishwa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa ambaye alimkumbusha Bw Odinga kuhusu jinsi jamii ya Wakamba imesimama naye katika chaguzi tatu zilizopita na anafaa “kurudisha mkono”.