Joto la kisiasa lapanda Tanzania Lissu akirejea

Joto la kisiasa lapanda Tanzania Lissu akirejea

NA MASHIRIKA

DODOMA, TANZANIA

JOTO la kisiasa limeanza kupanda Tanzania makamu Mwenyekiti wa chama cha Chadema Tundu Lissu akiwasili leo Jumatano.

Lissu ambaye pia alikuwa akipeperusha bendera ya Urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, alikuwa uhamishoni Ubelgiji.

Inafuatia tangazo la Rais Samia Suluhu Hassan mwezi huu – Januari – kwamba marufuku ya mikutano ya kisiasa yaliyowekwa na mtangulizi wake mwenye msimamo mkali yataondolewa.

Wiki jana, Lissu alisema kwamba atarejea nchini kuanza ukurasa mpya wa maisha.

Lissu, alipigwa risasi 16 katika jaribio la kutaka kumuua mwaka 2017.

Aliondoka nchini kuelekea Ubelgiji mwaka 2020 baada ya uchaguzi ambao Rais Magufuli alishinda kwa asilimia 84.

Uchaguzi wa 2020, hata hivyo, ulikumbwa na madai ya udanganyifu.

“Hiki kimekuwa kipindi kirefu na kigumu sana katika maisha yangu binafsi na katika maisha yetu kama chama na kama taifa. Hata hivyo, nitawasili Tanzania Januari 25,” alisema Lissu kwenye mahojiano ya hapo nyuma.

Lissu ambaye alikuwa mbunge wa Singida Kaskazini, alisafirishwa Kenya baada ya jaribio la kutaka kumuua mjini Dodoma Septemba 2017, na baadaye kusafirishwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Lissu alipigwa risasi mara kadhaa akiwa nyumbani kwake alipokuwa akitoka kwenye kikao cha bunge. Washambuliaji wake hawajawahi kukamatwa.

Hata hivyo, inaonekana kuna mapambazuko mapya kisiasa Tanzania hasa baada ya mwanasiasa huyo kudai kwamba hangeendelea kuishi Ubelgiji kwa muda usiojulikana.

Katika hotuba yake mnamo Januari 14, Lissu alibainisha kuwa lolote litakalotokea, mwaka huu utakuwa mwaka muhimu sana katika historia ya Tanzania.

“Ni mwaka ambao tukiamua, tutapata Katiba mpya na ya kidemokrasia yenye mfumo huru wa uchaguzi, unaojali na kulinda haki za wananchi na kuweka msingi imara wa uwajibikaji wa viongozi wetu kwa wananchi na wawakilishi wao,” alisema.

Alisema tayari Rais Samia Suluhu Hassan na chama chake cha CCM pamoja na Serikali yake wamejiweka hadharani kuwa wapo tayari kupata Katiba Mpya.

“Kama alivyosema Rais Suluhu, nasi tuko tayari na tumejipanga kwa ajili ya safari hiyo. Mimi binafsi na chama chetu tuko tayari na tumejiandaa kwa safari hiyo. Kwa hiyo narudi nyumbani kwa ajili ya kupata Katiba Mpya,” aliongeza mwanasiasa huyo.

“Ninarudi nyumbani ili kushiriki katika kuandaa ukurasa mpya wa kwanza wa Katiba chenye kurasa 365.”

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Watahiniwa waliozoa gredi za chini wasife...

UFUGAJI: Wachina huwania nyama ya sungura wao kila wakati

T L