Habari za Kitaifa

Jowie apatikana na hatia ya kumuua Monicah Kimani

February 9th, 2024 3 min read

RICHARD MUNGUTI Na HASSAN WANZALA

MAHAKAMA imewahukumu washtakiwa wawili wa mauaji ya mfanyabiashara Monicah Kimani usiku wa Septemba 19, 2018.

Akitoa hukumu Ijumaa, Jaji Grace Nzioka alisema japo upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kikamilifu kwamba mshukiwa mkuu Joseph Irungu almaarufu Jowie alihusika katika kifo cha mfanyabiashara huyo, lakini vitendo vyake siku chache kabla ya mauaji hayo, mienendo yake siku yenyewe ya mauaji na saa chache baadaye, vinamfunga.

“George Kimani alisema kwamba marehemu dadake alikuwa anamjua Jowie lakini mshtakiwa huyo mkuu alisema hakuwa anamfahamu,” akasema jaji Nzioka.

Koplo Jonathan Limo alikagua data za nambari ya simu ya Joseph Irungu Kuria na nyingine mbili za Monicah Nyawira Kimani.

Bi Nzioka alisema koplo Limo alithibitisha kwamba Jowie alikuwa akijuana na marehemu kabla ya kutokea kwa kifo chake.

Dominic Bisera Harun alisema aliacha kadi ya kitambulisho katika eneo la Royal Park Estate, Langata mnamo Septemba 17, 2018.

Mahakama ilithibitisha kwamba Bw Bisera alipoteza kitambulisho.

Shahidi mmoja alisema kitambulisho baadaye kilitolewa katika lango la kuingia kwa makazi ya marehemu.

Mahakama ilifahamishwa kwamba japo kulikuwa na utata kuhusu mavazi aliyovaa mshtakiwa wa kwanza, baadaye ilifanikiwa kuona kitambaa cheupe kilichochomeka na kwamba ilikuwa kanzu.

Mashahidi kadhaa walisema walimuona Jowie akiwa amevalia kanzu.

Shahidi Lee Owen alisema Jowie alikuwa katika makazi ya Monicah na pia alikuwa akizungumza kwa lugha msimbo.

Pia mahakama imenukuu maneno ya Jowie akiwa kwa nyumba ya marehemu.

Alisema: “Tofauti na mataifa mengine ambapo kila jambo huwajibikiwa, hapa Kenya mambo ni tofauti kwa sababu unaweza kufanya chochote na ukajiendea zako kwa sababu hakuna kanzidata za kufuatilia.”

Jowie alikuwa na bunduki ya Brian Kasaine na kwamba hakuwa ameirejesha kwa zaidi ya siku mbili.

Kuhusu gari la na mtangazaji Jacque Maribe, mahakama imesema lilionekana katika barabara ya Denis Pritt, karibu na makazi ya marehemu yaliyoko Lamuria Gardens.

Mashahidi walisema Jowie alikuwa akitumia gari hilo.

Licha ya ushahidi huo wote, mahakama ilisema haingeweza kumpata na hatia Jowie kwa msingi wa gwaride la utambulisho kwa sababu halikuendeshwa ipasavyo.

Akijifanya Harun, Jowie aliingia kwa makazi saa tano usiku na dakika 21 na kutoka baada ya dakika 10.

Lakini mahakama ilisema kutoka kwa kituo kimojawapo cha petroli ambapo Jowie alikuwa saa mbili na nusu usiku kufika kwa makazi ya marehemu, ni mwendo wa robo saa.

Shahidi mwingine alisema tofauti na nakala za kumbukumbu kwamba aliingia kwa makazi hayo saa tano za usiku, ‘ukweli’ wake ni kwamba Jowie alikuwa kwa makazi hayo saa tatu za usiku.

“Mshtakiwa wa kwanza aliiba kitambulisho cha Harun siku mbili kabla ya kifo cha Monicah. Pia mashahidi walisema alibeba begi kuashiria ilitumika kubeba kanzu. Pia alikosa kurudisha kwa wakati bunduki aliyokodisha. Aidha, mtaalamu alisema marehemu alikuwa na majeraha yaliyokuwa dhahiri kwamba yalitekelezwa na mtu mwenye ujuzi mkubwa,” akasema Bi Nzioka.

Uamuzi katika kesi dhidi ya wapenzi hao wa zamani uliahirishwa kusomwa mnamo Oktoba 6, 2023, Desemba 12, 2023, na Januari 26, 2024.

Mnamo Januari 26, 2024, Maribe hakufika kortini kwa vile alikuwa mgonjwa.

Lakini mnamo Ijumaa, Maribe alikuwa mwenye furaha tele baada ya mahakama kumuondolea shtaka la kutekeleza mauaji.

Jaji alisema Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) inaweza ikamfungulia mashtaka kwa kumdanganya afisa wa serikali.

Jacque Maribe na mpenziwe wa zamani Joseph Irungu almaarufu Jowie wakiwa kizimbani kupokea uamuzi katika kesi ya mauaji ya Monicah Kimani baina ya Septemba 19 na Septemba 20, 2018. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Maiti ya Monicah ilipatikana ndani ya karai katika bafu la nyumba yake eneo la Lamuria Gardens ikiwa imefungwa mikono na majeraha ya kukatwa shingoni.

Ushahidi uliowasilishwa ulisema Jowie ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na Monicah ndani ya makazi yake.

Hatimaye Jowie alijipiga risasi ya bega na kuumia na kuchoma nguo alizokuwa amevalia usiku huo lakini kinyasa alichovalia akiwa kwa Monicah kilikuwa na damu iliyofanyiwa utafiti wa maabara ikalingana na ile ya Monicah.

Jaji Nzioka alisema ushahidi uliowasilishwa na wakili wa Serikali Gikui Gichuhi umewahusisha na mauaji ya Monicah.

Wawili hao walipokuwa wasomewe uamuzi wa kesi hiyo Januari 26, 2024, Bi Maribe hakufika kortini ikabidi Bi Nzioka aeleze kwa kina sababu za kuahirisha kesi hiyo kuondoa dhana kulikuwa na njama au mchezo uliokuwa ukiendelea kuhusu kutosomwa kwa uamuzi huo wa mauaji ya kinyama ya Monicah Kimani katika makazi yake eneo la Lamuria Gardens mtaa wa Kilimani Nairobi.

“Nilikuwa tayari kusoma uamuzi wa kesi hii. Uko tayari. Nimetathmini ushahidi katika kurasa 2,000 na nilikuwa tayari kuusoma,” alisema Jaji Nzioka aliyefahamishwa na wakili Katwa Kigen anayemwakilisha Maribe kwamba mshtakiwa huyo aliugua.

Kesi hiyo ilipotajwa Ijumaa uamuzi kusomwa, Bw Kigen alifichua “mteja wangu Maribe hajafika kortini kwa vile ni mgonjwa na hawezi kufika kortini”.

Bw Kigen aliomba uamuzi huo uahirishwe kumwezesha Bi Maribe kufika kortini kuupokea.

“Mtu akiwa mgonjwa hawezi fuata na kuelewa kinachojiri. Naomba kwa mara ya kwanza uamuzi katika kesi dhidi ya Maribe na Jowie uahirishwe kumwezesha apone,” Bw Kigen alimsihi Jaji Nzioka.

Jaji huyo aliwaita mawakili Kigen na Prof Nadwa na David Ayuo wanaowakilisha Bi Maribe na Jowie mtawalia katika ofisi na kuwataka wamfikishe mwanahabari huyo kortini “hata kama yuko kwa hali gani.”

Jaji huyo aliwaeleza mawakili hao kwamba alikuwa tayari kuusoma uamuzi huo hiyo Januari 26, 2024.

Mawakili walimpendekezea ausome uamuzi huo kwa njia ya mtandao ili Bi Maribe aufuate popote alipokuwa wakati huo lakini Jaji Nzioka akakataa akisema “lazima washtakiwa wote wawe kortini.”

Uamuzi katika kesi dhidi ya wapenzi hao wa chanda na pete wa zamani uliahirishwa kusomwa mnamo Oktoba 6, 2023, na Desemba 12, 2023.

Jaji Nzioka alifafanua nyakati hizo mbili hangeusoma kutokana na sababu ambazo hangeweza kuziepuka.

Mara ya kwanza alikuwa mgonjwa na mara ya pili alipelekewa stakabadhi za ushahidi katika mahakama ya Naivasha anakohudumu ili azikague kabla ya kuandika uamuzi huo.