Habari Mseto

Jowie sasa ageukia usanii wa nyimbo za injili

August 21st, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Bw Joseph Kuria Irungu almaarufu ‘Jowie’ mshukiwa mkuu katika mauaji ya mfanyabiashara Monicah Kimani amegeukia usanii, miezi kadhaa baada ya kuachiliwa kwa dhamana na mahakama.

Jowie aliachiliwa Februari 2020, baada ya kuzuiliwa rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja. Alishtakiwa pamoja na aliyekuwa mpenzi wake mwanahabari Jacqueline Maribe, kufuatia mauaji ya kinyama ya Monicah usiku wa Septemba 19, 2018. Bi Maribe alikuwa ameachiliwa awali, kabla ya Jowie.

Miezi kadhaa baada ya kuachiliwa kwa dhamana ya Sh2 milioni pesa taslimu, ambazo alisaidiwa na marafiki kuchanga, Jowie sasa ni mwanamuziki wa nyimbo za injili.

Aidha, Jowie amezindua kibao ‘Nishikilie’, ambacho kimeonekana kuashiria maisha magumu aliyopitia wakati akiwa kizuizini, wimbo anaoelekeza mahitaji na matumaini yake kwa Mwenyezi Mungu.

Kwenye utangulizi wa ngoma hiyo, anaanza kwa kunukuu Somo la Biblia, Zaburi 31:15 “Maisha yangu yamo mikononi mwako, uniokoe kutoka mikononi mwa maadui zangu na wanaonidhulumu.”

Akionekana katika eneo kame, akiwa amelala, anaamka, Jowie anamsihi Mwenyezi Mungu; “Nishikilie…Mimi siwezi bila wewe…Nishike…Nishikilie…Mwamba ni salama…

Mwanamuziki huyo ambaye tutamtaja kuwa ni chipukizi katika nyimbo za injili, anaendelea kueleza Mola kwamba anazifahamu pandashuka zake zote. “Wewe wazijua, miteremko na pandashuka…Machozi yangu wewe wanipanguza…” Jowie anaimba kwenye kanda hiyo ya video na sauti.

Inapogonga dakika ya pili, Jowie anaelekea aliko mtoto wa kike aliyevalia rinda la samawati (buluu), na aliye na ala ya gitaa. Msichana huyo, anaungana naye kuimba huku akicheza ala hiyo ya muziki.

Kwenye mahojiano na mwigizaji na mtangazaji Felix Odiwuor almaarufu ‘Jalang’o’ kupitia mtandao wa Facebook Live, BONGA NA JALAS, Jowie Irungu alifichua kuingilia usanii wa nyimbo za injili.

Alisema msichana anayeonekana kwenye kibao chake cha kwanza ‘Nishikilie’, ni bintiye na kwamba ana mke.

Akitamatisha wimbo huo wenye urefu wa dakika 4 na sekunde 36, Jowie anatazama juu kueleza imani yake kwa Mwenyezi Mungu, “Yawe nakuamini Baba.

Kufikia sasa, kibao hicho kimeonekana kutazamwa na zaidi ya watu 100, 000 kwenye mtandao wa You-Tube.