JOY KINYUA: Serikali ipige jeki uigizaji nchini

JOY KINYUA: Serikali ipige jeki uigizaji nchini

Na JOHN KIMWERE

NI miongoni mwa wasanii wa kike wanaozidi kuvumisha tasnia ya filamu nchini. Ingawa amehitimu kama mwana habari wa televisheni anasema alitamani kuwa mwigizaji tangia akiwa mtoto.

Dada huyu Joy Wawira Kinyua maarafu kama Afande Supuu anadokeza kuwa uigizaji umeibuka taaluma yake tangu akamilishe elimu ya Chuo Kikuu mwaka 2018.

”Kusema ukweli tangu nikiwa mtoto nilikuwa napenda uigizaji maana yupo mmoja kati ya wanafamilia wetu alikuwa akishiriki masuala ya maigizo jambo lililonivutia zaidi,” alisema na kuongeza kuwa jkatika jukwaa hili analenga kuibuka miongoni mwa maprodusa mahiri nchini kama Wanuri Kahiu ama Judy Kibinge kati ya wengine.

Anadokeza kwamba akiwa mdogo alivutiwa zaidi na waigizaji wawili Catherine Kamau Karanja ‘Selina’ na Ida Alisha ‘ Olive’ walikuwa wakishiriki kipindi cha Mother Inlaw cha Citizen TV.

Binti huyo anasema akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu pia alikuwa akihudhuria masomo ya uigizaji katika shirika la Sanaa Acting, Yaya Centre ambapo ndipo alibahatika kukutana naye Abel Mutua ambaye ni kati ya wakurungezi maarufu wa filamu hapa nchini.

Binti huyu anayejivunia kushiriki filamu ya ‘Anda kava’ ambayo hupeperushwa kupitia Maisha Magic Plus na Maisha Maisha East ameshiriki filamu nyingi tu tangu mwaka 2013. Anda Kava hutengenezwa na Phil-it Production.

Kisura huyu anajivunia kushiriki vipindi kadhaa zilizobahatika kupeperushwa kupitia runinga kadhaa hapa nchini ikiwamo ‘Hapa Kule News'(KTN), ‘Mchungaji’ (NTV), ‘Baba Yao'(KTN), ‘Sue and Johnny’ ‘Varshita’, na ‘Ma Empress’ zote (Maisha Magic East).

Katika mpango mzima anasema badala ya waigizaji wa Kenya kuwazia kushiriki filamu za Hollywood katika mataifa ya kigeni wanastahili kuwa mstari wa kwanza kutengeneza zao za kiwango hicho. ”Wakenya tunafanya kazi nzuri kinyume na ilivyokuwa miaka iliyopita. Pia tunahitaji sapoti ya serikali na watazamaji wetu kama ilivyo katika mataifa yanayoendelea.”

Mfano serikali ya Nigeria imejenga vyumba vya wasanii kurekodia filamu zao ambazo hukodishiwa kwa ada nafuu ili kuwapiga jeki. Kusema kweli kama tasnia ya uigizaji inaweza kupata sapoti nzuri hapa nchini inaweza kuibuka kati ya sekta inayoletea serikali fedha nyinyi.”

Dada huyu anasema anatosha mboga ambapo amepania kufuata nyayo za mwigizaji wa kimataifa, Taraji P. Henson kati ya wasanii walioigiza katika filamu kama ‘Empire’ na ‘Acrimony’ miongoni mwa zinginezo.

Pia anasema kwa sasa yupo kwenye mchakato wa kuanzisha brandi ya kuzalisha filamu ambapo ndani ya miaka mitano ijayo anatakuwa akimiliki brandi yake pia akiwa produsa.

Anashauri wenzie wawe makini zaidi katika masuala ya maigizo hasa kila mmoja afahamu anachohitaji. ”Ninafahamu kuwa kwa wanawake kama sio mapenzi ya kushiriki filamu inakusuma kujiunga na sekta hii sina shaka kutaja kuwa hautadumu kwa muda mrefu,” akasema.

Anasema waigizaji wa kike hupitia pandashuka nyingi tu hasa wakati wanaume wengi hupenda kuwashusha hadhi na kuwataka kimapenzi ili kuwapa nafasi za ajira. Anasema mara kadhaa amenyimwa nafasi ya ajira baada ya kupotezea ombi la kuwa na mahusiano ya kimapenzi na maprodusa wawili tofauti.

You can share this post!

CLARA VUGUTSA: Nalenga kuwapa mafunzo ya uigizaji wasanii...

NEOLIN MOMANYI: Hongera NMG kwa kujitolea kuangazia masuala...