Makala

JOY WANGUI: Mwigizaji na DJ mtajika

July 25th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

ANATAMANI kuibuka kati ya waigizaji bora wa kike humu nchini na kimataifa miaka ijayo. Anaorodheshwa kati ya wasanii chipukizi ambao wameamua kujituma katika masuala tofauti kusaka riziki.

Joy Njeri Wangui maarufu VJ Ciara alianza kushiriki uigizaji mwaka 2015 baada ya kuvutiwa na tasnia hiyo tangu akiwa mdogo.

”Ingawa nimejikuta katika masuala ya burudani nikiwa mdogo nilitamani kuhitimu kuwa mwana habari wa televisheni ama redio,” alisema na kuongeza kuwa taaluma anazoshiriki ameamua kuzikumbatia kwa mikono miwili. Binti huyu anajivunia kuwa mwigizaji, video vixen bila kuweka katika kaburi la sahau DJ.

Anadokeza kuwa alivutiwa na uigizaji alipotazama filamu ya mwigizaji wa Nollywood, Jackie Appiah iitwayo ‘Beyonce’. ”Ninashiriki uigizaji nikilenga kutinga hadhi ya mwanamaigizo wa kimataifa mzawa wa Mexico, Maite Perroni aliyeshiriki Triumph of Love Soap Opera,” anasema.

Katika utangulizi wake katika masuala ya maigizo alifanya na kundi la Penyevu Arts. Kisura huyu ameshiriki filamu ya ‘Ngazi’ na ‘Uber Driver Maisha ya Mjini,” (My Dubai Date Cancelled EP10 na Nairobi Classy Lady encounter with bedbugs, kunguni balaa uber taxi driver EP15).

Ngazi aliyoshiriki kama nesi ilipeperushwa kupitia Rembo TV ilhali Uber Driver huonyeshwa kupitia mtandao wa Youtube. Kwa waigizaji wa humu nchini anasema angependa kufanya kazi na wasanii kama ‘Brenda Wairimu-filamu Mali,’ na Nyce Wanjeri-filamu Auntie Boss,’ kati ya wengineo. Duniani anatamani kushirikiana na waigizaji kama Lupita Nyong’o (Kenya)-filamu Black Panther na Jackie Appiah (Ghana)-filamu Beyonce.

VIXEN

Katika taaluma ya Video Vixen aliyoanza kushiriki mwaka jana anajivunia kushiriki nyimbo kadhaa ikiwamo ‘Kwa shida na raha-Staminah Gust FT Red C,’ ‘Caroline -Mr Bloom,’ ‘Deserve it-Russian Young,’ ‘Wanna-Kingwabz,’ ‘Good Loving-DJ Gogez featuring Kabagazi and Jerry Ogalo,’ na Kwachua-Nadhifu.’

U-DJ

”Kiukweli napenda masuala ya muziki nakumbuka nilianza kutunga nyimbo nikisoma kidato cha pili pia kufanya mixture,” alisema na kuongeza kwamba alianza masuala ya U-DJ mwaka 2016. Katika mpango mzima anasema masuala ya burudani ya muziki yalimvutia tangia akiwa mdogo.

”Binafsi nilitamani sana kuwa miongoni mwa kundi la Madj wachache wa kike kudhihirishia wenzetu kwamba tunaweza,” akasema.

Amefanya kazi na kumbi mbali mbali hapa nchini ikiwamo Club 17-Kahawa West, Landmark Gardens-Bypass, 7 Knights-Kimathi Street Nrb, Texas Inn-Maua, Dolce Tavern na 83 Place -Ngong Road kati ya zingine.

Pia amefanya kwenye harusi mbali mbali nchini bila kuweka katiuka kaburi la sahau kwenye za kitaifa za Mashujaa dei katika Kaunti ya Mombasa mwaka jana. Kadhalika amewahi kushiriki shoo ya Mwigangaro (Inooro TV).

MPANGO

Anasema anadhamiria kufungua akademia yake kufunza masuala ya U-DJ. Msichana huyu aliyezaliwa mwaka 1995 anashukuru mamake mzazi, Alice Wangui maana amekuwa mstari wa kwanza kumpa sapoti katika taaluma zake.

Anashauri wenzie kuwa wenye talanta kamwe hawapaswi kuvunjika moyo mbali wanastahili kujituma bila kulegeza kamba. Pia wanastahili kujiwekea mpango kabambe hasa kutimiza azma fulani ndani ya muda fulani.

Anashukuru wafuasi wake kwa kumpa sapoti katika kazi zake tangu alipokuwa msanii chipukizi na kusema wamemjenga pakubwa kisanaa. Kadhalika anawaomba waendelee kumpa sapoti na endapo hawatamuangusha atazidi kuwaandalia kazi nzuri na ya kuvutia.