Makala

JOYCE OTIENO: Ielewe biashara ya uanamitindo

July 25th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

WAHENGA waliposema penye nia pana njia hawakudanganya maaana ndivyo ilivyo tangu zama hizo mpaka sasa. Msemo huo umeonyesha mashiko ya haja miongoni mwa jamii.

Hili linazidi kudhihirishwa na vijana wengi, wavulana na wasichana ambao wameamua kujituma kisabuni kwenye juhudi za kusaka riziki.

Joyce Branice Otieno ni kati ya wana mitindo wanaokuja hapa nchini wanaolenga kufikia upeo wa kimataifa miaka ijayo.

”Kiukweli ningependa sana kushiriki masuala ya mwana mitindo kufikia kiwango cha kimataifa miaka ijayo,” alisema na kuongeza kwamba anafahamu bayana kwamba hakuna kizuri hupatikana rahisi lazima mtu ajitume kiume ili kutimiza ndoto yake.

Msichana huyu anadokeza kuwa ni jukumu la kila mmoja wao kujihusisha na taalamu yeyote hasa anapohisi ndipo talanta yake ilipo ili kupata namna ya kujipatia riziki. Hayo tisa. Kumi msichana huyu amehitimu kwa cheti cha mhudumu wa ndege.

LUPITA NYONG’O

Dada huyu anasema katika masuala ya uanamitindo angependa sana kufuata nyayo za mwana dada mahiri mzawa wa Nigeria, Folake Kuye maarufu kama Style Pantry. Ingawa hajapata mashiko katika taaluma ya uanamitindo anasema anaamini ana uwezo wa kufanya vizuri.

Ingawa tangu utotoni mwake alitamani kuhitimu kuwa mwimbaji msichana huyu anasema alivutiwa na masuala ya uanamitindo baada ya kumtazama mwigizaji wa Kenya, Lupita Nyong’o anayetamba katika uigizaji nchini Marekani.

”Kiukweli Lupita ambaye ni pia mwana mitindo alinivutia kwa jinsi alivyoshiriki katika filamu ya Black Panther,” alisema na kuongeza kwamba anapania kufikia viwango vya kimataifa miaka ijayo maana kando na kutamani kuwa mwimbaji amekuwa na ndoto ya kuwa mwana mitindo.

Mwanzo wake mwaka jana alishiriki tangazo la biashara la kampuni iitwayo Sanlaam lililotengenezwa na shirika la Versatile Agency baada ya kujiunga nalo mwaka 2018. Tangazo hilo lilipeperushwa kupitia Citizen TV.

”Imekuwa vigumu kupata tangazo lingine kwa sababu kwenye shirika yupo wengi ambapo ni lazima kila mmoja apewe nafasi,” akasema.

Msichana huyu anasema katika taaluma ya uanamitindo angependa sana kufanya kazi na Celestine Gachuhi maarufu Selina anayejivunia kushiriki filamu ya Selina. Filamu hiyo ilipata mpenyo kupeperushwa kupitia Maisha Magic.

USHAURI

Binti huyu mwenye umri wa miaka 19 anasema anaamini kuwa uanamitindo ni kazi kama nyingine. Anadokeza kuwa licha ya kutopata nafasi kuonyesha uwezo wake anatarajia kuzipata hivi karibuni baada ya janga la virusi hatari vya corona kudhibitiwa.

”Tayari nimetuma nyaraka za kuomba ajira katika mashirika mbali mbali nchini,” alisema na kuongeza kuwa ana imani ipo siku milango yake itafunguka. Anashauri wasichana wenzake kwamba kwanza wajiamini kwa kila kitu wanachofanya pia wasitake tamaa maishani.