Joylove FC yapigwa jeki vifaa vya kuchezea

Joylove FC yapigwa jeki vifaa vya kuchezea

NA JOHN KIMWERE

KOCHA na mwanzilishi wa klabu ya Joylove FC, Joyce Achieng ameingia ushirikiano na UEFA Foundation for Children and Football4Wildlife kwenye jitihada za kupalilia vipaji vya wachezaji chipukizi.

Ameshukuru uongozi wa shirika hilo baada ya kupokea ufadhili wa vifaa mbali mbali vya kuchezea ikiwamo mipira 20, nyavu nane kati ya vifaa vingine vya kutumia wakati wa kushiriki mazoezi.

”Ninashukuru uongozi wa shirika hilo kwa ufadhili wa vifaa vya kuchezea maana vitawapa wachezaji wangu nafasi nzuri ya kushiriki mazoezi bila tatizo kwa muda,” amesema na kuongeza kuwa amepania kujadiliano na viongozi wa shirika hilo ili kufungua ofisi katika Kaunti Ndogo ya Dagoretti.

Kocha wa JOYLOVE, Joyce Achieng akionyesha vifaa vya kuchezea walivyopokea kutoka kwa UEFA Foundation for Children and Football4Wildlife. PICHA | JOHN KIMWERE

Joylove ina timu za wavulana na wasichana ambazo huchezea kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Gatina, Dagoretti Nairobi.

Timu ya wasichana hushiriki kampeni za Central Regional League (CRL) na wako mbioni kupigania tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi kujiunga na Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu ujao.

Warembo hao tayari wamekaa pazuri kubeba tiketi ya kupandishwa ngazi maana wako kileleni kwa kuzoa alama 27, nane mbele ya Kirigiti baada ya kushiriki mechi tisa na 11 mtawalia.

Baadhi ya wachezaji wa JOYLOVE FC. PICHA | JOHN KIMWERE

Joylove ina mechi nne kapuni nayo Kirigiti ina mechi tatu kapuni.

Timu hiyo inajivunia kukuza mchezaji mmoja, Nancy Wafula ambaye husakatia Limuru Starlets ya Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza. Kwa sasa wasichana hao wamekamata nafasi ya tano kwenye jedwali la kipute hicho.

 

  • Tags

You can share this post!

Mwongozo kusaidia wanahabari wa kike kukabili unyanyasaji...

Uongezaji thamani kwa maziwa unaimarisha kipato, wafugaji...

T L