Habari za Kitaifa

JSC yafutilia mbali uajiri wa majaji wapya 11 baada ya serikali kufinya mgao wake

Na SAM KIPLAGAT July 3rd, 2024 1 min read

TUME ya Huduma za Mahakama (JSC) imesitisha uajiri wa wafanyakazi wakiwemo majaj 11 wapya wa Mahakama ya Rufaa baada ya Hazina ya Kitaifa kubana matumizi ya fedha kwa shughuli zake kuwa asilimia 15 ya mgao wa bajeti kwa JSC.

Jaji Mkuu Martha Koome alisema kuwa taarifa kutoka Hazina ya Kitaifa imeagiza kuwa JSC itumie fedha kwa ‘huduma muhimu pekee’.

“Agizo hili litakuwa na athari kubwa katika utendakazi wa Idara ya Mahakama na JSC. Kwa hivyo, tunalazimika kufanya mabadiliko kwa mipango na shughuli za idara hii,” Jaji Koome akasema.

Idara ya Mahakama ilikuwa imetengewa Sh24 bilioni katika Bajeti ya Kitaifa iliyosomwa na Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u mwezi jana. Huo ni ongezeko la Sh1.2 bilioni, kutoka Sh23.2 bilioni ilizotengewa katika mwaka uliopita wa kifedha wa 2023/2024.

Katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023, Idara ya Mahakama ilitengewa Sh19.3 bilioni katika bajeti ya kitaifa.

Idara ya mahakama ilikuwa ikiomba itengewa fedha nyingi ili iweze kufadhili shughuli zake na kujenga majengo mapya ya mahakama kote.

Hata hivyo, baada ya kuingia mamlakani serikali ya Rais William Ruto iliahidi kuongeza mgao wa bajeti wa Idara ya Mahakama kwa Sh3 bilioni kila mwaka ili iweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Juzi, Rais Ruto alisema bajeti ya matawi yote ya serikali yatapunguzwa baada ya Wakenya kukatalia mbali Mswada wa Fedha wa 2024 ambao ulitarajia kuwezesha serikali kukusanya Sh347 bilioni zaidi kufadhili bajeti yake ya Sh3.9 trilioni.