Habari Mseto

JSC yakutana kusaka mrithi wa Maraga

February 19th, 2020 2 min read

Na JOSEPH WANGUI

TUME ya Huduma za Mahakama (JSC) Jumatano inatarajiwa kuandaa kikao kujadili masuala nyeti kuhusu Mahakama ya Juu na uhaba wa majaji katika Mahakama ya Rufaa.

Katibu wa JSC Anne Amadi jana alisema kuwa maandalizi ya kustaafu kwa Jaji Mkuu David Maraga si miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa kwenye kikao hicho.

Duru za kuaminika, hata hivyo, zilisema kuwa mipango ya kutafuta mrithi wa Jaji Mkuu Maraga itajadiliwa katika kikao hicho.

Kulingana na duru, tume itajadili bajeti ya mwaka wa fedha ujao utakaoanza Julai mwaka huu. Bajeti hiyo itajumuisha fedha zinazohitajika kumtafuta Jaji Mkuu mpya baada ya Maraga kustaafu mwaka ujao.

Lakini jana, Bi Amadi ambaye ni Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama alisema kuwa kikao cha leo kitajadili uajili wa maafisa wa Baraza la Kitaifa kuhusu utoaji wa Haki (NCAJ).

Jaji Mkuu Maraga anatarajiwa kustaafu Januari 2021 baada ya kufikisha umri wa miaka 70. Lakini wandani wake wanasema huenda akastaafu mapema mwishoni mwa mwaka huu sawa na alivyofanya mtangulizi wake, Dkt Willy Mutunga.

Iwapo Jaji Maraga ataamua kustaafu mapema, huenda shughuli za Mahakama ya Juu zitakwama kutokana na ukosefu wa idadi ya majaji wanaohitajika kusikiliza kesi.

Hii ni kwa sababu Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu hajawa akiketi kwenye jopo la majaji kwani anakabiliwa na kesi mbele ya JSC.

Aidha, Jaji Jackton Ojwang tayari ameenda likizoni akingojea kustaafu.

Shughuli za Mahakama ya Juu zimekuwa zikiendeshwa na majaji watano ambao ndio idadi ya chini inayohitajika; Jaji Maraga, Smokin Wanjala, Mohamed Ibrahim, Isaac Lenaola na Njoki Ndung’u.

Kesi dhidi ya Jaji Mwilu iliwasilishwa mbele ya JSC na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI).

Tume ya JSC itakutana Machi mwaka huu kusikiza kesi hiyo ambapo DCI na DPP wanataka Jaji Mwilu aondoke afisini.

Iwapo JSC itamuondoa, azma yake ya kumrithi Jaji Mkuu Maraga itasambaratika.

Mkurugenzi wa DCI George Kinoti Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji watatoa ushahidi dhidi ya Jaji Mwilu. Bw Haji alilazimika kumshtaki Jaji Mwilu mbele ya JSC baada ya jopo la majaji watano kuzima hatua yake ya kumshtaki kortini kwa madai ya kuhusika na uhalifu.

Jaji Mwilu pia alinusurika kushtakiwa mnamo Mei mwaka jana baada ya Mahakama Kuu kusema kuwa DPP na DCI walipata ushahidi dhidi yake kwa njia isiyofaa.

Bw Haji anadai kuwa Jaji Mwilu hafai kushikilia afisi ya umma kwa kushindwa kulipa ushuru na kughushi stakabadhi za kifedha.

Bi Amadi katika ripoti ya Idara ya Mahakama iliyotolewa wiki iliyopita, alisema JSC inatarajia kuajiri jaji mmoja wa Mahakama ya Juu, na majaji 30 wa Mahakama Kuu, Mazingira, Leba na Ardhi.

Tume ya JSC pia inatarajiwa kuajiri mahakimu 100 na wafanyakazi 300 katika idara ya mahakama kama hatua mojawapo ya kukabiliana na mrundikano wa kesi.