Habari

'Jua ni jinsi gani bajeti itakavyokuathiri'

June 13th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imetenga Sh10.7 bilioni kulipa malimbikizi ya madeni ambayo asasi za serikali zinadaiwa na wafanyabiashara, hasa wale wadogowadogo, amesema Waziri wa Fedha Henry Rotich.

Anasema madeni haya, yasiyo na maswali ya ukaguzi, yatalipwa kabla ya Juni 30, 2019, alivyoamuru Rais Uhuru Kenyatta juzi.

Wafanyabiashara wanaouza bidhaa kwa asasi za serikali sasa watakuwa wakilipwa baada ya siku 60, Rotich ameamuru.

Amezitaka serikali za kaunti kuiga mfano huo.

Magari yote ya serikali kununuliwa kutoka kwa watengenezaji wa magari wa humu nchini, bajeti inapendekeza. Rotich amesema hatua hiyo inalenga kupiga jeki sekta ya kiviwanda humu nchini; kulingana na maono ya Ajenda Nne Kuu za serikali.

  • Miradi ya Ajenda Nne Kuu yatengewa Sh450 bilioni kwa ujumla.
  • Mpango wa elimu bila malipo umetengewa Sh13.4 bilioni.
  • Elimu bila malipo katika shule za upili – Sh55.4 b
  • Sh2.3 bilioni za kuajiri walimu wapya.
  • Sh4 bilioni za mitihani ya kitaifa ya kufuzu elimu ya msingi na sekondari; KCSE na KCPE.
  • Sh97.7 bilioni kwa elimu ya vyuo vikuu
  • Sh12.6 bilioni kwa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELB).
  • Sh4 bilioni za bima ya matibabu kwa wanafunzi wa shule za upili za umma.
  • CDF imetengewa Sh49.7 bilioni

Hazina ya Usawazishaji inayosimamiwa na Wawakilishi wa Wanawake imetengewa Sh2.3 bilioni.

Hazina ya usawazishaji wa maendeleo (Equalization Fund) Sh5.8 bilioni

Pigo kwa waraibu wa mchezo wa Kamari ambapo sasa watalipa ushuru wa asilimia 10 kwa pesa zote wanachezea.

Sigara na mvinyo, ushuru wapandishwa pia. Bei za bidhaa hizi za burudani zitapanda.

Pia ni pigo kwa wanaofanya biashara ya bodaboda kwa sababu watahitajika kulipia abiria wao bima. Hatua hii waziri amesema itasaidia kupunguza ajali katika sekta hii ya uchukuzi.