Makala

TAHARIRI: Jubilee, heri uwanja mmoja kuliko nunge

February 22nd, 2020 2 min read

Na MHARIRI

HATAMU ya miaka 10 ya Serikali ya Jubilee imesalia na miaka miwili kabla ya kukamilika.

Ila katika sekta ya michezo, serikali hii haijalipa deni kubwa ‘ililokopa’ kutoka kwa wananchi. Deni lenyewe ni viwanja vitano vya hadhi ya kimataifa.

Hata hivyo, Wakenya kwa sasa wanafahamu fika kuwa haiwezekani kwa sasa, serikali ya Jubilee, yenye madeni chungu nzima, kujenga viwanja vitano.

Kwa hivyo, watafurahi sana kupata uwanja mmoja tu kuliko kutoka mikono mitupu. Serikali yetu yafaa iongozwe na tamathali inayosema heri nusu shari kuliko shari kamili.

Vilevile, serikali yoyote wajibifu inafaa itilie mkazo usemi kwamba ahadi ni deni na dawa yake ni kulipa. Katika hili, Wakenya hawahitaji kulipwa deni zima bali sehemu yake tu.

Wakijengewa hata uwanja mmoja tu, wataelewa kuwa japo serikali ilikuwa na matatizo yake ya kifedha, ilikuwa na nia njema kuhusu maisha ya vijana hasa wenye vipawa vya michezo.

Hata ingawa tunashukuru kwa serikali kuchukua hatua ya kukarabati na kuinua hadhi ya uwanja wa kitaifa wa Nyayo, itakuwa bora zaidi iwapo uwanja mpya wa kiwango cha juu utajengwa.

Swali linalofaa kuipiga serikali yetu mshipa ni je, inakuwaje kuwa mataifa madogo kiuchumi kama vile Rwanda na Tanzania yana viwanja vingi vya kisasa ilhali Kenya tunashindwa hata kuongeza uwanja mmoja tu?

Kenya ndiyo kitovu cha uchumi katika ukanda huu wa Afrika kiasi kwamba mataifa mengi jirani yamekuwa yakiitamani. Inakuwaje, hivyo basi, kuwa mambo madogomadogo kama ujenzi wa miundomsingi ya michezo yanatushinda?

Sharti tuzinduke usingizini, vinginevyo, tutajipata tumepitwa na kila mtu.

Umuhimu wa miundomsingi kama vile viwanja bora ni upi kwa raia na hasa wanamichezo? Wanamichezo watapata fursa ya kujiandaa vizuri na kukuza vipawa vyao.

Pia panapokuwa na miundombinu bora, kutokana na mvuto wa kimazingira, vijana wengi watajitosa viwanjani kwa ajili ya kukuza vipawa vyao na hivyo basi kufikia upeo wa kusajiliwa na klabu za hadhi nchini au kimataifa na hivyo kujipa riziki nzuri.

Kadhalika, nafasi nyingi za kazi zitajitokeza.