Na KENYA NEWS AGENCY
MBUNGE wa Kieni, Bw Kanini Kega amekana madai kuwa chama cha Jubilee kimekufa, akisema mipango ya kukiimarisha inaendelea.
Akiongea na wanahabari katika Shule ya Msingi ya Gitero katika eneobunge hilo Jumatano, Bw Kega alisema chama hicho kingalipo na kinaendesha shughuli kama kawaida.
Alisema chama hicho kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta ndicho cha pili kwa wingi wa wanachama.
“Jubilee ingali hai. Ndicho chama tawala na ukienda katika afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa utagundua kuwa imeorodheshwa ya pili kwa idadi ya wanachama nchini,” Mbunge huyo akasema bila kutaja chama chenye idadi kubwa zaidi ya wanachama nchini.
Bw Kega pia alisema Kongomano la Kitaifa la Wajumbe wa Jubilee (NDC) lililoahirishwa mnamo Desemba 10, 2021 litafanyika hivi karibuni.
“Chama cha Jubilee kinapanga kufanya NDC iliyoahirishwa mwishoni mwa mwaka 2021. Tunasubiri kupitishwa kwa Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Kisiasa ambao sasa uko katika seneti utiwe saini kuwa sheria kabla ya wajumbe wetu kuitwa,” Bw Kega akasema.
Alielezea imani kuwa maseneta watapitisha mswada huo akisema unasheheni mapendekezo mazuri yanayolenga kuimarisha usimamizi wa vyama vya kisiasa nchini.