Jubilee kuachia kila raia deni la Sh180,000

Jubilee kuachia kila raia deni la Sh180,000

Na BENSON MATHEKA

SERIKALI ya Jubilee itaachia kila raia wa Kenya, wakiwemo watoto watakaozaliwa mwaka 2022, mzigo wa kulipa Sh180,000 kwa sababu ya madeni inayoendelea kukopa.

Kufikia sasa, deni la Kenya ni Sh7.7 trilioni na kulingana na makadirio ya ukopaji unaotarajiwa, itaongeza Sh1.8 trilioni kufikia Juni 2022.

Ikizingatiwa kuwa idadi ya Wakenya inakadiriwa kuwa milioni 50, Jubilee itakapoondoka mamlakani mwaka 2022, kila Mkenya atakayekuwa amezaliwa atakuwa na deni la Sh180,000.

Tamaa ya madeni ya serikali ya Jubilee imefanya maisha ya Wakenya kuwa magumu huku ikitumia asilimia 85 ya ushuru inaokusanya kuyalipa.

Wizara ya Fedha iliambia bunge kwamba ilichukua mikopo 10 mipya ya jumla ya Sh293.5 bilioni kati ya Aprili 1 na Agosti 31, 2021.

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kwamba nusu ya mikopo hiyo italipwa na serikali ijayo, kumaanisha kuwa Wakenya hawatapata afueni baada ya Jubilee kuondoka mamlakani.

“Ilivyo ni kuwa Wakenya watalipa madeni ya serikali ya Jubilee miaka mingi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuondoka mamlakani. Huu ndio ukweli wa mambo,” mwanauchumi Silvester Ochuka aliambia Taifa Leo jana Alhamisi.

Kulingana na Mhasibu Mkuu wa serikali, Nancy Gathungu, serikali imeongeza madeni kwa asilimia 125 ikiwa ni kima cha asilimia Sh4.2 trilioni ndani ya miaka sita na kuyafanya kukaribia kiwango cha juu cha madeni, Sh9 trilioni, kilichowekwa na bunge.

Dkt Gathungu aliambia Kamati ya Fedha ya Seneti kwamba deni la Kenya la Sh7.7 trilioni ni asilimia 85 ya kiwango cha Sh9 trilioni ambacho wabunge waliweka 2019.

Kumekuwa na mipango ya kuongeza kiwango hicho hadi Sh12 trilioni, jambo ambalo wanauchumi wanasema bunge likipitisha, Jubilee itaacha nchi na zigo kubwa zaidi la madeni.

Asilimia 84 ya madeni ya Kenya yalikopwa na serikali ya Jubilee ilipoingia mamlakani 2013 ikiahidi kutekeleza miradi kabambe ya miundomsingi.

Kulingana na gazeti la Business Daily, serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imekopa zaidi ya Sh6.1 trilioni kwa miaka tisa ambayo imekuwa mamlakani.

Ilipoingia mamlakani mnamo 2013, deni la Kenya lilikuwa Sh1.79 trilioni. Ikiwa serikali itakopa Sh1.87 trilioni inavyokadiria, serikali ya Jubilee itakakuwa imekopa Sh2.5 bilioni kila siku na kuongeza deni la Kenya kuwa Sh8.06 trilioni mwishoni mwa mwaka huu.

Serikali inaendelea kubebesha Wakenya mzigo kwa kuwa inavyoendelea kulipa madeni ndivyo inavyoendelea kukopa zaidi kutoka katika taasisi za kifedha za kimataifa na za humu nchini.

Baadhi ya madeni huwa na masharti makali yanayoumiza raia.

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akitetea madeni ya serikali yake akisema yamesaidia kuimarisha miundomisingi nchini kama ujenzi wa reli ya kisasa, barabara na mabwawa.

Hata hivyo, madeni hayo yamekuwa ‘yakimeza’ nusu ya pesa ambazo serikali inakusanya kama ushuru na kuiacha ikitatizika kuendesha serikali na miradi ya maendeleo, elimu na idara ya afya. Deni hili linapotishia Wakenya, Dkt Gathungu anaibua maswali kuhusu rekodi za ulipaji mikopo hiyo akisema zinaonyesha kuna dosari.

Hasa, Mhasibu Mkuu huyo wa serikali anadadisi jinsi Sh2 bilioni zilivyotumika kwenye mwaka wa kifedha uliomalizika Juni 2020.

“Kulikuwa na Sh2 bilioni zaidi ambazo Benki Kuu ya Kenya (CBK) haikudhihirisha na huenda hazitapatikana,” alisema Dkt Gathungu.

Mwelekezi wa Bajeti, Margaret Nyakango pia ameibua maswali kuhusu jinsi mikopo hiyo ilivyotumiwa akisema kiwango kikubwa kilitumiwa kulipa madeni kinyume cha sheria ya Usimamizi wa Pesa za Umma ya 2012.

You can share this post!

Olunga butu Harambee Stars ikiona vimulimuli dhidi ya Mali

Ufaransa kukutana na Uhispania kwenye fainali ya UEFA...