Habari MsetoSiasa

Jubilee kukosa pesa za matumizi

September 11th, 2019 2 min read

Na BRIAN OCHARO

CHAMA cha Jubilee kimo hatarini kukosa fedha za matumizi ikiwa ombi lililowasilishwa kwa Jopo la Kusuluhisha Mizozo ya Chama litakubaliwa.

Afisa wa chama hicho katika Kaunti ya Mombasa, Bw Patrick Kabundu ameomba jopo hilo kutoa amri ya muda inayosimamisha afisi ya msajili kutoa fedha za vyama kwa Chama cha Jubilee hadi kesi yake itakaposikizwa na kuamuliwa.

Mlalamishi huyo alitaka pia amri ya kusimamisha mchango wa kila mwezi wa magavana, wabunge na madiwani wa chama hicho hadi kesi yake ikamilishwe.

Endapo jopo litakubali ombi hilo, huenda shughuli za Jubilee zikaathirika vibaya ikiwemo kufadhili kampeni za chaguzi ndogo zitakazoshiriki katika kipindi cha kesi hiyo.

Wakati huo huo, hatua yake imeashiria mikakati ya kumwondoa Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju katika usimamizi wa chama imeanza kushika kasi.

Bw Kabundu ambaye ni katibu wa chama hicho katika Kaunti ya Mombasa, anasema viongozi wa chama ambao pia ni wafanyakazi wa serikali wamekiuka Kipengele cha 77(2) cha katiba na wanafaa kutolewa katika nyadhifa hizo.

“Viongozi kama hao waliapishwa na kuahidi kuheshimu katiba lakini sasa wanaikiuka. Viongozi wa chama cha Jubilee wamekiuka kipengele hicho kwa kushikilia nyadhifa hizo huku wakiwa wafanyakazi wa serikali,” alisema.

Kipengele 77(2) cha katiba ya Kenya kinasema kuwa yeyote aliyeteuliwa kuhudumu serikalini hafai kushikilia ofisi katika chama cha siasa.

Bw Kabundu ameomba jopo hilo kutoa amri kuwa wale wanaohudumu serikalini waondoke katika nyadhifa za chama kwani wameenda kinyume na katiba.

Ameambia jopo hilo la Bw Kyalo Mbobu, Bi Milly Lwanga na Dkt Adelaide Mbithi kuwa chama cha Jubilee hakifuati katiba ya Kenya na hata ya chama kiusimamizi, na kuwa jopo hilo linahitajika kutoa amri chama hicho kifuate sheria.

“Viongozi wote wa Chama cha Jubilee ni wafanyakazi wa serikali. Hii ni kinyume cha sheria,” akasema.

Jopo hilo limepatia chama hicho kinaochoongozwa na Rais Kenyatta muda wa siku 10 kujibu malalamishi ya Bw Kabundu. Kesi hiyo itasikizwa Septemba 27.

Bw Tuju ambaye ni Waziri asiyesimamia wizara yoyote, amekuwa akikashifiwa na wanachama wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, wanaodai ana ubaguzi.

Hivi majuzi, aligonga vichwa vya habari aliposema orodha ya wagombeaji ubunge Kibra ambao walitaka tikiti ya chama hicho iliyowasilishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikuwa feki, licha ya kwamba ilionekana kuwa na sahihi iliyodhaniwa kuwa yake.

Mnamo Juni, alijikuta taabani na kikundi cha Tangatanga kinachomshabikia Dkt Ruto wakati mawasiliano ya simu kati yake na Bw George Nyanja yalipofichuliwa, wakizungumzia njama zinazoweza kutumiwa kumhangaisha Naibu Rais kisiasa.

Bw Kabundu analaumu chama hicho kwa kukosa kuleta umoja wa wanachama huku akidai kuwa kuna migawanyiko ambayo inaweza kusababisha chama hicho kukosa kutekeleza wajibu wake wa kisiasa.

Mlalamishi ameambia jopo hilo kuwa chama cha Jubilee kimekataa kutii notisi iliyotolewa na msajili wa chama ambayo ilitaka viongozi wanaoshikilia nyadhifa serikalini wang’atuke kwenye vyeo vya vyama.