Na CHARLES WASONGA
CHAMA cha Jubilee sasa kinapania kuvunja uhusiano wake na chama cha Party of Reforms and Development (PDR) kilichobadilishwa jina na kuwa United Democratic Alliance (UDA), na kuhusishwa na Naibu Rais William Ruto.
Katika hatua inayoonekana kulenga kumlemaza kisiasa Dkt Ruto, Jubilee imemwandikia barua msajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu ikiomba kuzima mkataba wa ushirikiano kati yake na PDR wa Mei 2018.
Kwenye taarifa iliyotolewa Aprili 20, 2021 Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alisema Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi (NMC) ya chama hicho tawala ilisema ilifikia uamuzi huo kwa sababu PDR imebadili maafisa, nembo, falsafa na hata jina.
“PDR ambacho kimebadilika kuwa UDA sasa ni adui ya Jubilee kwa sababu kulingana na mkataba wa awali chama hicho kilipaswa kudhamini wagombeaji katika kaunti ya Pokot Magharibi, Wajir, Isiolo, Garissa na Mandera pekee. Lakini sasa kinashindana na Jubilee katika kaunti nyingine jinsi ilivyoshuhudiwa Nakuru na sasa Nyandarua na Kisii,” akasema Bw Tuju.
Katibu huyo mkuu ambaye alifafanua kuwa anawasilisha msimamo wa kamati ya NMC, alisema Jubilee imeamua kuchukua hatua hiyo kwa sababu UDA kinaendeleza ajenda ya uhasla.
“Vile vile, Jubilee imekatiza mchakato wa kukamilishwa kwa uundwaji wa muungano inavyohitajika kulingana na Sheria ya Vyama vya Kisiasa,” akasema.
“Hata hivyo, wanachama wa muungano huo uliovunjwa ambao wanashikilia nyadhifa za uongozi katika mabunge mbalimbali wataendelea kuhudumu katika nyadhifa hizo, ilivyopangwa katika mkataba wa Mei 2018,” Bw Tuju akafafanua katika barua hiyo.
Hii ina maana kuwa Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo aliyechaguliwa kwa tiketi ya PDR na anashikilia wadhifa wa naibu kiongozi wa wengi katika Seneti ataendelea kuhudumu katika wadhifa huo katika bunge hilo. Madiwani waliochaguliwa kwa PDR pia wataendelea kushikilia nyadhifa zao katika mabunge ya kaunti za Wajir, Mandera, Isiolo na Garissa.