Jubilee yaachia NASA chaguzi ndogo

Jubilee yaachia NASA chaguzi ndogo

Na CECIL ODONGO

CHAMA cha Jubilee kimeendelea na mtindo wake wa kutowawasilisha wawaniaji kwenye ngome za washirika wake, baada ya kutangaza jana kuwa hakitawadhamini wagombeaji katika chaguzi ndogo za maeneobunge ya Kabuchai, Matungu na useneta wa Machakos.

Wapigakura wa Kabuchai na Matungu kwenye Kaunti za Bungoma na Kakamega mtawalia wataelekea debeni mnamo Machi 4, 2021 kuwachagua wawakilishi wapya huku wale wa Machakos wakimchagua seneta mpya hapo Machi 18, 2021.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju jana alisema chama hicho kimewaachia washirika wake kwenye handisheki ODM, Ford Kenya, Wiper na ANC wamenyane katika chaguzi hizo ndogo, ambazo zimebashiriwa kuwa ubabe kati ya vigogo wa vyama hivyo na Naibu Rais William Ruto katika ngome zao.

“Chama cha Jubilee hakitawasilisha wawaniaji wake kwenye chaguzi ndogo katika maeneobunge ya Kabuchai, Matungu na Useneta wa Machakos. Hii ni kwa sababu kwa sasa tunajivunia ushirikiano wa kuridhisha na washirika wetu ODM, ANC, Wiper na vyama vingine,” akasema Bw Tuju.

Jubilee haikuwa na mgombeaji wa kiti cha ubunge wa Msambweni mnamo Desemba mwaka jana, na badala yake ilimuunga mkono mwaniaji wa ODM Omar Boga ambaye alibwagwa na mwaniaji huru Feisal Bader.

Dkt Ruto na wandani wake walimuunga mkono Bw Bader na walitaja ushindi huo kama ishara ya kudidimia kwa umaarufu wa kinara wa ODM Raila Odinga ukanda wa Pwani.

“Uamuzi huu wa Jubilee unalenga kuhakikisha umoja wa taifa hasa kupitia ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI),” akaongeza Bw Tuju.

Alisema kuwa chama hicho hata hivyo, kitawasilisha wawaniaji kwenye chaguzi ndogo katika wadi za Hell’s Gate na London katika Kaunti ya Nakuru na ile ya Huruma, Kaunti ya Uasin Gishu.

Katika wadi ya London, Francis Njoroge Njogu atapeperusha bendera ya Jubilee huku Virginia Wamaitha na Lucy Njoroge wakidhaminiwa kugombea katika wadi za Hell’s Gate na Huruma mtawalia.

Bw Tuju pia alibainisha kwamba chama hicho bado hakina mgombeaji wa kiti cha ugavana katika Kaunti ya Nairobi kwa kuwa bado kinasubiri utata unaozingira kuandaliwa kwa kura hiyo uamuliwe na mahakama kuu.

Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais, tayari kimewateua Alex Lanya kama mgombeaji wake katika eneobunge la Matungu huku Evans Kakai akipeperusha bendera ya chama hicho kipya Kabuchai.

UDA pia imemtangaza aliyekuwa mbunge wa Starehe Askofu Margaret Wanjiru kuwa mwaniaji wake katika kiti cha ugavana wa Nairobi na inatarajiwa kumtangaza mgombeaji wao hivi karibuni kuwania Useneta Machakos.

Mbunge wa zamani David Weru wa ODM naye atamenyana na Peter Nabulindo wa ANC, pamoja na Bw Lanya eneo la Matungu. Hapo jana, Wiper nayo ilimtangaza Agnes Kavindu, aliyekuwa mke wa seneta wa zamani Johnstone Muthama, apeperushe bendera yake katika Kaunti ya Machakos.

Kwa upande mwingine, Ford Kenya ya Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula ambayo ina umaarufu sana katika kaunti za Bungoma na Trans Nzoia wiki jana ilimtangaza Majimbo Kalasinga kama mwanizi wake Kabuchai.

Bw Wetang’ula alisema chama hicho ambacho ni cha pili kwa ukongwe zaidi nchini baada ya Kanu, hakitawasilisha mwaniaji Matungu na badala yake kitaunga mkono Bw Nabulindo.

ANC pia itarudisha mkono kwa kuunga mkono Bw Kalasinga kule Kabuchai. Viti vya ubunge vya Kabuchai na Matungu vilisalia wazi baada ya mauti ya wabunge James Lusweti na Justus Murunga.

Kile cha Useneta wa Masaku nacho kilibakia bure baada ya kifo tatanishi cha Boniface Kabaka.

You can share this post!

Polisi wengi wagura kazi, walia wanalipwa mshahara wa kitoto

FAUSTINE NGILA: Kukwamilia WhatsApp ni ithibati Afrika...